

Tanzania na Morocco zakubaliana kuimarisha ushirikiano wa matumizi ya teknolojia katika Sekta ya Nishati ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na mchango endelevu nchini.
Hayo yamebainishwa Mei 14, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati alipokutana na mwenyeji wake Waziri wa Mageuzi ya Nishati na Maendeleo Endelevu wa Ufalme wa Morocco, Mhe. Leila Benali kuzungumza kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati ili kuimarisha ushirikiano na nchi ya Morocco.
“Mwaka 2016 Tanzania na Morocco zilisaini hati ya makubaliano (MoU) ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya umeme, mafuta na matumizi ya nishati mbadala ili yapewe kipaumbele katika nchi hizo”. Amesema Dkt. Biteko
Mhe. Dkt. Biteko amesema pamoja na maendeleo ya nishati yaliyofikiwa, bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati mbadala ikiwa na matarajio ya kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda na madini jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati.
Kwa upande wake, Waziri wa Mageuzi ya Nishati na Maendeleo Endelevu wa Ufalme wa Morocco, Mhe. Leila Benali amesema kuwa Tanzania inaweza kubadilisha sura yake kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha, Mhe. Benali amepongeza kwa dhati juhudi za Rais Samia kuwa kinara wa maendeleo ya nishati safi ya kupikia, Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Dennis Londo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ally Mwadini, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Africa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Rosemary Jeiro, wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!