Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Sekretarieti ya Mbowe Yajiondoa Chadema, Wasema Chama Kimepoteza Mwelekeo – Video

  • 46
Scroll Down To Discover

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Benson Kigaila

Dar es Salaam — Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Benson Kigaila, ametangaza kujiondoa rasmi ndani ya chama hicho akidai kuwa kimepoteza mwelekeo na misingi ya demokrasia. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano, Kigaila alisema kuwa yeye pamoja na wenzake waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA taifa wameamua kuachana na chama hicho kutokana na kile alichokieleza kuwa ni kukosekana kwa uongozi wa kidemokrasia na kufuatwa kwa katiba ya chama.

“Sisi tumeamua wote kwa pamoja kujiondoa CHADEMA ili tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka, kwa sababu sisi hatuwezi kuwa sehemu ya chama ambacho maamuzi yake hayafanywi kwa vikao, hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambacho wanachama wanabaguliwa, hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambacho katiba haifuatwi,” alisema Kigaila kwa hisia kali.

Kigaila aliongeza kuwa wao sio “chawa” bali ni viongozi wanaojitambua ambao waliingia CHADEMA kwa malengo ya kuleta mabadiliko ya kidemokrasia nchini. Hata hivyo, alidai kuwa chama hicho kimepoteza malengo hayo na sasa kimegeuka kuwa taasisi inayofanya maamuzi kwa misingi ya ubaguzi na upendeleo.

“Kwahiyo tunajitoa CHADEMA ili wasipate sababu kwamba chama hiki kilikufa kwa sababu tulikuwepo. Tunataka kuwaachia waendeshe wanavyotaka. Sisi sio wazee wa kustaafu, tutaendelea kuwapigania Watanzania na tutatafuta jukwaa muafaka,” aliongeza.

Kigaila hakufafanua juu ya mwelekeo wao mpya wa kisiasa baada ya kujiondoa CHADEMA, lakini alisisitiza kuwa wataendelea kupigania maslahi ya wananchi kwa namna wanayoona inafaa.

Kujiondoa kwa Kigaila kunakuja siku chache baada ya mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho, ambapo viongozi kadhaa wa ngazi za juu waliondolewa kwenye nafasi zao katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika Januari 22, 2025. Hatua hii imeibua sintofahamu na mjadala mzito kuhusu mustakabali wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.



Prev Post EWURA Yatangaza Bei Mpya za Mafuta ya Petroli na Dizeli
Next Post Shigongo Aongoza Waombolezaji Kumuaga Kasango Mwizalubi, Buchosa- Video
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook