
Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania (TEC) Padri Dkt. Charles Kitima ameripotiwa na Vyanzo mbalimbali vya habari kuwa amevamiwa na kushambuliwa na watu wasiofahamika, akiwa kwenye makazi yake, zilipo Ofisi za baraza hilo Kurasini Jijini Dar Es salaam majira ya saa tatu na nusu usiku wa Aprili 30, 2025.
Mara baada ya shambulizi hilo, Padri Kitima amepatiwa matibabu ya awali kwenye Kituo kidogo cha afya cha TEC kilichopo eneo hilo na baadaye kusaidiwa na baadhi ya watu kupandishwa kwenye gari tayari kupelekwa kwenye Hospitali ambayo mpaka taarifa hii inaandaliwa bado haikuwa imefahamika ni Hospitali gani alipoenda kupatiwa matibabu.
Padri Kitima kando ya utumishi wake na nafasi aliyonayo ndani ya Kanisa, amejipatia umaarufu mkubwa nchini Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni kwa namna ambavyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa mienendo isiyofaa kwenye jamii na akiwa mstari wa mbele katika kuhubiri utawala wa sheria na haki za binadamu pamoja na Demokrasia.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!