
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kwa kushirikiana na Kampuni ya Target Tours and Labour Supply Limited, imetangaza nafasi 470 za ajira katika fani mbalimbali za ujenzi nchini Falme za Kiarabu (UAE), kupitia Kampuni ya DHCN General Construction L.L.C – S.P.C iliyopo Abu Dhabi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi hiyo, Watanzania wenye sifa zinazohitajika wametakiwa kutuma maombi ya nafasi hizo kuanzia Oktoba 27 hadi Novemba 3, 2026.
NAFASI ZA KAZI ZILIZOTANGAZWA
Nafasi hizo zimegawanywa katika kada saba za kazi za ujenzi kama ifuatavyo:
- Fundi Rangi (Painter) – Nafasi 30.
- Fundi Mchundo (Steel Fixer) – Nafasi 50.
- Fundi Seremala (Carpentry) – Nafasi 50.
- Fundi Bomba (Pipe Fitter) – Nafasi 80.
- Msaidizi wa Fundi (Helper) – Nafasi 120.
- Fundi Viunzi (Scaffolder) – Nafasi 80.
- Fundi Uchomeleaji (Welder) – Nafasi 60.
Jumla ya nafasi zote ni 470, huku nafasi nyingi zaidi zikiwa za wasaidizi wa mafundi, ambazo ni 120.
SIFA ZA WAOMBAJI
Waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya msingi au sekondari, pamoja na uzoefu wa angalau mwaka mmoja katika fani husika, ikiwemo uchoraji, uchomeleaji, useremala, ufundi bomba, ufungaji wa vyuma na viunzi.
Aidha, mwombaji anatakiwa kuwa na uwezo wa kuzungumza na kuandika lugha ya Kiingereza, kuwa mwanamume na kuwa na umri wa miaka 21 hadi 45.
MASHARTI YA AJIRA
Kwa mujibu wa tangazo hilo, mshahara utalipwa kulingana na sheria za nchi ya Falme za Kiarabu.
Gharama za matibabu kwa kipindi chote cha ajira zitagharamiwa na mwajiri, ambaye pia atashughulikia viza ya mfanyakazi.
Vilevile, mwajiri atagharamia tiketi ya kurudi baada ya kukamilika kwa mkataba wa miaka miwili, pamoja na malazi na chakula katika kipindi chote cha mkataba.
Mwajiri pia atagharamia usafiri wa kutoka nyumbani hadi kituo cha kazi kwa kipindi chote cha ajira.
MUDA NA MAHALI PA USAILI
Waombaji wanapaswa kuwasilisha maombi yao kuanzia Oktoba 27 hadi Novemba 3, 2026.
Usaili umepangwa kufanyika Novemba 9, 10 na 11, 2026, katika Chuo cha VETA, Dar es Salaam.
JINSI YA KUTUMA MAOMBI
Waombaji wanatakiwa kutuma wasifu binafsi (CV) kupitia tovuti ya Kampuni ya Target Tours and Labour Supply Limited kwa anuani ya www.targettours.co.tz au kupitia barua pepe info@targettours.co.tz.
Baada ya kutuma maombi, waombaji wanapaswa kujisajili kupitia Mfumo wa Kazi Portal ili kukamilisha mchakato wa maombi, kwa kutumia anuani ya https://jobs.kazi.go.tz.

The post Serikali Yatangaza Nafasi 470 za Kazi za Ujenzi Nchini Falme za Kiarabu appeared first on Global Publishers.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!