Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ili kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kumpokea Rais wa Kenya, William Ruto, aliyewasili nchini kwa ziara ya kitaifa, Rais Samia amesema mazungumzo yao yamelenga zaidi masuala ya kiuchumi yanayogusa ustawi wa mataifa hayo.
Katika ziara hiyo, mikataba nane imesainiwa ikihusisha sekta za nishati, miundombinu na uchukuzi, TEHAMA, kilimo na biashara, ulinzi, ambapo Rais Samia ameeleza kuwa katika sekta ya ulinzi Tanzania na Kenya zimekubaliana kuongeza ulinzi na umakini zaidi kwenye mipaka, ili watu wenye nia ovu wasivuke na kufanya uovu katika nchi hizo.
“Tumezungumza kufanya vizuri kwenye mipaka yetu, kuongeza ulinzi, kuongeza umakini kwenye mipaka yetu ili watu waovu wasiwe wanavuka kufanya uovu upande wowote ule kati ya nchi zetu mbili,” amesema.
Kwa upande wa miundombinu, amebainisha kuwa makubaliano yamefikiwa ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, pamoja na kuunganisha reli kutoka Bandari ya Tanga kupitia Kilimanjaro hadi Kenya. Pia, Kenya itaunganisha reli yake na kipande cha Reli ya Kisasa (SGR) cha Tanzania kutoka Singida.
Kwa upande wa Rais wa Kenya, William Ruto amesema Tanzania na Kenya zinahitajiana hivyo zinapaswa kuimarisha ushirikiano zaidi kwa kujenga madaraja badala ya vikwazo, na kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi na wafanyabiashara wa nchi zote mbili.
The post Tanzania na Kenya zakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi appeared first on SwahiliTimes.






Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!