

Dodoma, Novemba 11, 2025 — Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanza rasmi vikao vyake leo kwa kufanyika kwa kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya.
Kazi kubwa inayotarajiwa kufanyika katika kikao cha leo ni uchaguzi wa Spika wa Bunge, ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia alikuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita, Mussa Azzan Zungu, anapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho.
Sambamba na hilo, wabunge pia watafanya uchaguzi wa Naibu Spika, nafasi ambayo kwa mujibu wa taarifa za ndani, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, anatajwa kuwa kinara katika mbio hizo.
Baada ya kukamilika kwa chaguzi hizo, Bunge litafanya kazi ya kuidhinisha jina la Waziri Mkuu, kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kulizindua rasmi Bunge hilo jipya.
Vikao hivi vinatarajiwa kuweka msingi wa shughuli za Bunge la 13, ambalo litakuwa na wajibu mkubwa wa kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, na mipango ya maendeleo ya taifa katika kipindi kijacho cha miaka mitano.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!