

Mwanza, Oktoba 28, 2025 — Mgombea Mwenza wa Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesisitiza kuwa atakuwa mkono thabiti wa Mgombea Urais wa CCM, akihakikisha maono na utekelezaji wa ilani ya chama kwa kipindi cha miaka mitano ijayo yafanikishwe kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za CCM katika Uwanja wa Kirumba, Mwanza, Dkt. Nchimbi alisema:
“Nakushukuru sana Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama chetu cha CCM kwa imani yako kubwa kwangu kwa kunipendekeza kuwa msaidizi wako mkuu. Miaka minne iliyopita uliniteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, kisha ukanipendekeza kuwa Katibu Mkuu wa CCM na sasa umeniamini katika nafasi ya Mgombea Mwenza.”

Dkt. Nchimbi aliendelea kueleza kuwa:
“…ndani ya miaka minne umeonesha imani yako kwangu kwa kunipa nafasi muhimu ndani ya Taifa letu na ndani ya CCM. Nakuhakikishia kuwa imani uliyoonesha, namna pekee ninayoweza kuilipa ni kukusaidia kwa nguvu, akili, maarifa na uaminifu ili ndoto na maono yako na utekelezaji wa ilani yetu ya CCM (2025/30) ufanyike kwa mafanikio makubwa katika miaka mitano ijayo.”
Mgombea Mwenza huyo pia alibainisha kuwa wananchi wa Tanzania wameridhika na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25 na wameridhia kazi ya Mgombea Urais:
“…hilo linatokana na utendaji kazi wako katika Serikali ya Awamu ya Sita unayoiongoza inayotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Watanzania katika sehemu zote tulizopita wameridhika na wamesema kuwa kesho watakupa kura nyingi za ushindi wa kishindo.”
Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka Mwanza na maeneo jirani, huku ukijazwa kwa shauku, nyimbo za kampeni na hamasa ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!