

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imesema kuwa imezuia “njama kubwa” ya kumpindua kiongozi wa jeshi, Kapteni Ibrahim Traoré, ambapo jeshi limedai kuwa waliopanga njama hiyo walikuwa wakifanya kazi hiyo kutoka nchi jirani ya Ivory Coast.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema jaribio hilo la mapinduzi liliongozwa na wanajeshi wa sasa na wa zamani waliokuwa wakishirikiana na “viongozi wa kigaidi”. Aliongeza kuwa lengo lao lilikuwa kushambulia ikulu ya rais wiki iliyopita.
“Mpango huo ulikuwa na dhamira ya kusababisha machafuko makubwa nchini, na kuiweka nchi chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa,” alisema Sana kupitia televisheni ya taifa siku ya jana Jumatatu.
Hii ni miongoni mwa madai kadhaa ya njama za kumng’oa madarakani kiongozi huyo wa kijeshi aliyechukua mamlaka mwaka 2022 wakati mashambulizi ya waasi yalipokuwa yakiongezeka.
Burkina Faso, kama majirani zake wa ukanda wa Sahel, imekuwa ikipambana na makundi yenye silaha ya wanajihadi, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya eneo la nchi hiyo liko chini ya udhibiti wao.
Licha ya ahadi za serikali ya kijeshi ya Kapteni Traoré za kuboresha hali ya usalama na hata kutafuta ushirikiano mpya wa kiusalama na Urusi, hali bado ni mbaya kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa waasi.
Na Elvan Stambuli, GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!