

Serikali ya Jamhuru ya kidemokrasia ya Congo, DRC, imesema imesimamisha chama cha Rais wa zamani Joseph Kabila, siku chache baada ya mali zake kuvamiwa na maafisa wa usalama.
Katika taarifa, wizara ya usalama wa ndani ya DRC ilisema kwamba uamuzi huo unafuatia uanaharakati uliozidi wa Kabila, aliyehudumu kama Rais kwa miaka 18 hadi mwaka 2019 na ambaye amesalia kuwa kiongozi wa chama cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).
Wizara hiyo ilifafanua kwamba shughuli zote za chama cha PPRD aimesimamishwa katika sehemu zote za taifa hilo. Chama hicho hata hivyo hakikujibu hatua hiyo ya serikali mara moja.
Rais Felix Tshisekedi amemlaumu Kabila kwa kuandaa kile alichokitaja kuwa uasi na kuunga mkono makundi yanayojumuisha M23 ambalo linapigana na wanajeshi wa serikali mashariki mwa DRC.
Kabila mwenye umri wa miaka 53, aliondoka nchini DRC kabla ya uchaguzi wa Urais mwaka 2023,kulingana na msemaji wa familia yake. Hata hivyo amerudi nchini kwake na inadaiwa alitembelea mji wa Goma unaoshikiliwa na waasi wa M23 kwa kupitia nchini Rwanda. Anadaiwa hajalaani waasi hao.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!