
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ndani wa kupokea na kuchambua wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Gabriel Makalla, chama hicho kimeeleza kuwa mchakato huo utaanza tarehe 1 Mei 2025, saa 2:00 asubuhi na kumalizika tarehe 15 Mei 2025, saa 10:00 jioni.
Zoezi hilo linahusisha utoaji na urejeshaji wa fomu kwa wanachama wanaotaka kugombea nafasi za Ubunge, Udiwani, na Uwakilishi kupitia makundi mbalimbali ya chama hicho kama vile UWT, UVCCM, na WAZAZI pamoja na makundi maalum ya wafanyakazi, wasomi, NGOs, na watu wenye ulemavu.
Utaratibu wa kuchukua na kurejesha fomu ni kama ifuatavyo:
Ubunge na Baraza la Wawakilishi (wote): Wanachama watachukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM wilaya husika.
Viti Maalum (kupitia UWT): Wanachama wanawake watarudisha fomu kwa Katibu wa UWT Mkoa.
Viti Maalum (kupitia UVCCM): Wanachama vijana wanawake watarudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM Mkoa.
Viti Maalum (kupitia WAZAZI): Wanachama wanawake watarudisha fomu kwa Katibu wa WAZAZI Mkoa.
Udiwani (Bara na Zanzibar): Fomu zitachukuliwa na kurejeshwa kwa Katibu wa CCM Kata/Wadi.
Udiwani Viti Maalum (wanawake): Fomu zitachukuliwa na kurejeshwa kwa Katibu wa UWT Wilaya.
Taarifa hiyo pia imehimiza wanachama kufuata utaratibu uliowekwa na kuhakikisha fomu zinajazwa kikamilifu ndani ya muda uliopangwa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!