
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inalaani kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kupelekea matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro hali inayopelekea ukatili uliokithiri kwa binadamu hususani watoto, wanawake, wazee pamoja na wagonjwa katika maeneo ya migogoro.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani. Amesema uwepo wa mitazamo ya kibeberu, ikiwa ni pamoja na ile ya kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya uchukuaji rasilimali na uporaji wa ardhi, pamoja na uwepo wa makampuni ya kimataifa kuendelea kufanikiwa kutokana na unyonyaji wa mali asili za Afrika, huku wakisababisha au kuunga mkono migogoro inapaswa kumalizika sasa.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inauchukulia msimamo wa upande mmoja na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi, pamoja na kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani katika kukomesha umwagaji damu na vita vya hatari vinavyoendelea katika maeneo mengi duniani, kuwa ni jambo lisilokubalika.
Pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa ongezeko la matumizi ya fedha katika masuala ya kijeshi ikiwemo utafiti na utengenezaji wa silaha ni jambo la kusikitisha na ni kinyume cha maadili. Amesema hali hiyo inazuia jitihada za kutafuta amani duniani, na inachukua kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo zingeweza kutumika kuendeleza maendeleo endelevu na ustawi kwa wanadamu wote.
Makamu wa Rais amesema dunia inapaswa kuendelea kutafuta amani bila kuchoka kwani ndio sharti la maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amepongeza juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia, na mashirika ambayo yanashiriki kikamilifu katika upatanishi na utatuzi wa migogoro katika nchi na maeneo kama vile Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Urusi, Ukraine, na Mashariki ya Kati. Ametoa wito wa ushirikishwaji kamili wa wanawake katika kutafuta amani hususani katika kipindi hiki inaposherehekewa miaka 30 tangu azimio la Beijing na maendeleo yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!