MAGAZETI ya Leo Jumapili 30 Machi 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu, Utumishi, Juma Mkomi kuhakikisha barua za waliopita kwenye usaili na kupangiwa vituo vya kazi zinatolewa kwenye mikoa husika walikofanyia usaili badala ya kuwalazimu kusafiri hadi Dodoma Sekretarieti ya Ajira kufuata barua hizo.
Amesema kitendo cha watumishi hao wapya kupatiwa barua katika mikoa husika kitasaidia kupunguza gharama, usumbufu pamoja na muda wanaoutumia kufika hadi Dodoma.
Simbachawene ametoa maelekezo hayo Machi 29, 2025 jijini Dodoma wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Akitolea mfano Simbachawene amefafanua kuwa mwananchi amefaulu usaili Mkoa wa Kigoma anaifuata barua Dodoma ambapo anakuta amepangiwa tena mkoa huohuo.
“Barua hizo wachukulie kwenye mikoa walikofanyia usaili makatibu tawala, wataalamu wenye maadili wa kufanya kazi hiyo wapo, hivyo tuwape dhamana waifanye,” amesisita Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu, Utumishi, kuandaa kituo cha pamoja (One Stop Centre) katika ofisi hiyo kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi wa umma, ikiwa ni ubunifu wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo papo kwa hapo kwa watumishi wenye changamoto za kiutumishi wanaofika Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!