

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb), ametembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), na kutoa pongezi kwa TTCL kwa kazi nzuri ya kuimarisha huduma za mawasiliano nchini.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mahundi alipokelewa na viongozi waandamizi wa TTCL pamoja na Timu ya Wataalamu wa shirika hilo ambao walimpa maelezo ya kina kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo huduma ya intaneti ya kasi kupitia mtandao wa Faiba Mlangoni, miundombinu ya kitaifa ya NICTBB na huduma za kidijitali kupitia Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja (Call Center).

Mhe. Mahundi alionesha kufurahishwa na namna TTCL inavyotekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma muhimu kwa wananchi, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchina kuongeza kuwa TTCL imeendelea kuwa nguzo muhimu katika sekta ya mawasiliano kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za intaneti, simu na data katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Nawapongeza TTCL kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuimarisha mawasiliano. Mnafanya kazi kubwa ya kuisaidia serikali kufikisha huduma kwa wananchi. Nimefurahishwa pia na uchapakazi wenu kama watumishi wa TTCL ambavyo mmeonesha weledi katika kutekeleza majukumu yenu,” alisema Mhe. Mahundi.
Aidha, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiamini TTCL na kutumia huduma zake kwani ni kampuni ya kizalendo inayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kupitia miundombinu ya mawasiliano salama na ya kisasa.
Kwa upande wake, viongozi wa TTCL walimshukuru Mhe. Mahundi kwa kutembelea banda hilo na kuahidi kuendelea kuboresha huduma ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko na dira ya maendeleo ya Taifa la kidijitali.
Ziara ya Mhe. Mahundi imeongeza hamasa kwa watumishi wa TTCL na kuthibitisha imani ya serikali kwa shirika hilo la kihistoria linaloendelea kuwa daraja la mawasiliano ya kisasa kwa Watanzania wote.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!