
Mwanamuziki nguli wa Rock na Heavy Metal, Ozzy Osbourne, maarufu kama ‘Prince of Darkness’, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76. Taarifa rasmi kutoka kwa familia yake imethibitisha kuwa alifariki akiwa amezungukwa na familia yake na watu wa karibu, tukio lililotikisa dunia ya muziki.
Ozzy alikuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, ikiwemo ugonjwa wa Parkinson pamoja na matatizo ya mgongo yaliyotokana na ajali ya pikipiki ya ATV mwaka 2003, hali iliyomfanya apunguze shughuli za kisanii katika miaka ya mwisho ya maisha yake.
Kabla ya kifo chake, Osbourne aliaga rasmi jukwaa kupitia tamasha lake la mwisho lililofanyika Julai 5, 2025, kwa jina la kihistoria ‘Back to the Beginning’, ikiwa ni heshima kwa safari yake ya muda mrefu na ya kipekee katika muziki.
Ozzy Osbourne atakumbukwa kama mmoja wa vinara wa Heavy Metal, aliyelitikisa jukwaa kupitia bendi ya Black Sabbath kabla ya kuanzisha safari ya mafanikio kama msanii wa kujitegemea. Uwezo wake wa kipekee wa kisanii, sauti ya kipekee, na mvuto wake wa jukwaani vilimpa nafasi ya kipekee katika historia ya muziki wa dunia.
Wadau wa muziki, mashabiki na wanamuziki wenzake kote duniani wameendelea kumlilia gwiji huyo, wakimtaja kama mtu aliyeacha alama isiyofutika.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!