
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewapongeza Watumishi na Uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kufanikiwa kuandika historia mpya ya makusanyo ya Kodi kwa kuvuka malengo kwa miezi 12 mfululizo katika mwaka wa Fedha 2024/2025.
Akifungua kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuweka mikakati ya kufanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 jijini Arusha leo tarehe 08/07/2025 Waziri Mkuu amesema kazi iliyofanywa na TRA imefanikishwa na lugha moja inayozungumzwa na Watumishi pamoja na Uongozi wa TRA ndiyo maana wamekusanya Sh. Trilioni 32.26 sawa na asilimia 103 ya lengo la Sh. Trilioni 31.5.
Amesema Serikali inatambua, inaheshimu na inathamini kazi kubwa inayofanywa na TRA na ipo tayari kuiondolea vikwazo vya kisera, kisheria na kikanuni kama vipo ili iendelee kufanya vizuri huku akiwafikishia salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mkuu amesema mafanikio makubwa yanayoonekana yanatoa picha kwamba TRA imeendelea kufanya kazi kwa kujali uzalendo ambayo ndiyo njia sahihi ya kufika kwenye mafanikio.
“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa TRA kila unapohitajika ili iendelee kufanya vizuri na kusaidia kuhamasisha wananchi kujua umuhimu wa kulipa Kodi” amesema Waziri Mkuu.
Amesema nchi inaitegemea TRA katika kuiwezesha kutekeleza shughuli za maendeleo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!