

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuhakikisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yanaimarishwa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na sekta binafsi, wajasiriamali na wawekezaji ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 07 Julai 2025, alipofungua rasmi Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza mafanikio ya TanTrade na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuendeleza maonesho hayo na kuyaweka katika viwango vya kimataifa. Amebainisha kuwa mwaka huu, maonesho hayo yamevutia zaidi ya washiriki 5,734 kutoka ndani na nje ya nchi, jambo linalodhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara barani Afrika.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amezitaka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na TanTrade kuhakikisha kuwa elimu kuhusu Nembo Maalum ya Taifa kwa bidhaa na huduma za Tanzania (MADE IN TANZANIA) inawafikia wazalishaji na wananchi ili kuchochea uzalendo wa kibiashara.
Amesema uzinduzi rasmi wa nembo hiyo unalenga kuongeza thamani na kutambulisha ubora wa bidhaa za nchi katika soko la kimataifa.
Mapema, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi alitembelea mabanda ya maonesho ya kampuni za biashara na huduma kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na kukutana na wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi alikabidhi zawadi kwa kampuni bora yaliyofanya vizuri zaidi katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba 2025, pamoja na Wadhamini Wakuu wa maonesho hayo.
Halikadhalika, alipokea tuzo maalum pamoja na ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zao katika kuimarisha maonesho hayo pamoja na kukuza mikakati ya biashara na uwekezaji nchini. Sambamba na hilo, Rais Dkt. Mwinyi alizindua rasmi Nembo Maalum ya Taifa kwa bidhaa na huduma za Tanzania, MADE IN TANZANIA.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!