

Dar es Salaam, Julai 2, 2025
Msafara wa baiskeli wa Twende Butiama mwaka 2025 umeanza rasmi leo jijini Dar es Salaam, ukiwa na waendesha baiskeli zaidi ya 200 waliojitolea kushiriki safari hii ya kihistoria ya zaidi ya kilomita 1,500 kwa muda wa takribani siku 11 kutoka jijini Dar es Salaam mpaka mji wa Butiama.
Tukio hili linafanyika kama sehemu ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye urithi wake wa fikra na maono unaendelea kuiongoza Tanzania.
Jana, washiriki walikusanyika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere ili kupata baraka kutoka kwa mjane wake, Mama Maria Nyerere, ikiwa ni ishara ya kuaga kwa heshima kabla ya kuanza safari.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Agapinus Tax, Mkurugenzi wa `Viatarishi na Uzingatiaji wa Sheria kutoka Vodacom Tanzania, alieleza kuwa msafara wa mwaka huu utapita katika mikoa 11 na utahusisha waendesha baiskeli wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi.
“Zaidi ya waendesha baiskeli 200 watashiriki safari hii kutoka Dar es Salaam hadi Butiama. Kati yao, 50 watarudia njiani huku 150 wakitarajiwa kufika hadi mwisho wa safari,” alisema.
Msafara wa mwaka huu umekusanya washiriki kutoka kila kona ya Tanzania ikiwemo Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Mbeya, Kagera, Dodoma, Pwani na Tabora, pamoja na wale wa kimataifa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Botswana, DRC, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Marekani, Uholanzi na Nigeria.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, msafara wa Twende Butiama umetoa mafanikio makubwa ikiwemo kupanda miti zaidi ya 100,000, kufikia watu 23,000 kupitia huduma za afya kwa njia ya kliniki tembezi, kugawa madawati 1,900 kwa shule 32 za umma, na kutoa baiskeli 50 kwa wanafunzi waishio mbali na shule.
Mwaka huu, waandaaji wanalenga kufikia shule 10 zaidi, kupanda miti 50,000, na kuwafikia Watanzania zaidi ya 700,000 wakiwemo watoto, vijana na wazee.
Akizindua rasmi tukio hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema kuwa msafara huu si tu kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, bali pia ni chombo muhimu cha kuhamasisha afya na maendeleo ya jamii:
“Msafara huu ni kumbusho la umoja na uzalendo. Washiriki wanapata fursa ya kujifunza historia kwa njia ya vitendo. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa sekta za michezo, utamaduni na jitihada za kulinda mazingira,” alisema.
Naye Mwanzilishi Mwenzake wa msafara huo, Gabriel Landa, alieleza kuwa safari hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii zenye kugusa maisha ya wananchi, zikiongozwa na maono ya Mwalimu ya kupambana na ujinga, maradhi na umasikini.
“Waendesha baiskeli watashiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti kwenye maeneo ya Mlima Kilimanjaro na chanzo cha Mto Pangani ili kusaidia kuhifadhi mazingira,” alibainisha.

Kwa upande wake, Wilmot Ishengoma, Mkuu wa Idara ya Hatari kutoka Benki ya Stanbic Tanzania, alisisitiza mchango wa msafara huo katika kuhamasisha maisha yenye afya na ushiriki wa jamii:
“Msafara huu unaendelea kuhamasisha jamii, hasa katika kuhimiza mazoezi na afya njema,” alisema
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!