KATIKA kile kinachoonekana kuwa mwanzo wa ukurasa mpya kwa klabu ya Yanga, uongozi wa timu hiyo umeweka wazi mikakati kabambe ya kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi imara zaidi kwa ajili ya mashindano yote yaliyo mbele yao.
Mjumbe wa Yanga, Alex Ngai ameeleza dhamira yao ya kufanya usajili bora na wa kimkakati.
Hatua hiyo inakuja baada ya kuondoka kwa kiungo nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki, ambaye amejiunga na klabu ya Wydad AC ya Morocco.
Ngai amesema , klabu hiyo ililazimika kumuuza mapema kutokana na ukweli kwamba alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja tu uliosalia, na kuamua kufanya biashara mapema kabla hajatoka bure.
“Tumemuuza mapema ili tupate kitu, huu ni mpira wa kisasa na lazima tuwe wafanyabiashara wazuri,” amesema kiongozi huyo.
Katika hatua ya kuziba pengo la Aziz Ki, taarifa zinaeleza kuwa Yanga ipo katika hatua nzuri za mazungumzo na kiungo wa Singida Black Stars, Arthur Bada, ambaye anatajwa kuwa chaguo la kwanza kuchukua nafasi hiyo.
Arthur ni mmoja wa viungo wenye uwezo mkubwa wa kushambulia na kusaidia ulinzi, kitu ambacho kinaendana na falsafa ya Yanga kwa sasa.
Akizungumzia mipango ya msimu ujao, kiongozi huyo Ngai amesema:“Msimu ujao tutakuwa na usajili bora kabisa. Tutaleta wachezaji ambao si tu wana uwezo, bali wana njaa ya mafanikio wale wanaoweza kutufikisha mbali zaidi kimataifa.”
Aidha, ameongeza kuwa Yanga haitakubali tena kudhulumiwa na watu aliowaita “wahuni” na kwamba klabu hiyo itahakikisha inasimama kidete kutetea haki zake, huku ikilenga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Ngai amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa na mshikamano, kuwaunga mkono viongozi wao na kuhakikisha wanakuwa wamoja katika kila hatua ya safari ya mafanikio.
“Tusigeukane. Tuungane, tusimame pamoja. Mbele yetu kuna ushindi mkubwa kama tukidumu kwenye umoja,” amesema.
The post MRITHI WA AZIZI KI YANGA HUYU HAPA….MABOSI WAANZA KUFANIKISHA DILI MAPEMAAA…. appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!