Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

Wiki ya AZAKI 2025 Kuanza na Mjadala Kuhusu Dira ya Maendeleo 2050

  • 42
Scroll Down To Discover

Arusha, 1 Juni 2025 – Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) kwa mwaka 2025 itafunguliwa rasmi Jumatatu tarehe 2 Juni katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, ikiwa na ajenda kabambe inayolenga kujadili njia zitakazoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati wa ngazi ya juu ifikapo mwaka 2050.

Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, anatarajiwa kuhutubia hafla ya kufunga maadhimisho hayo ambayo yatahitimishwa Ijumaa tarehe 6 Juni 2025. Wiki ya AZAKI 2025, ikiwa na kaulimbiu isemayo “Njia gani tunaweza kutumia ili kufikia maendeleo,” inaonesha dhamira ya Asasi za Kiraia ya kuoanisha Dira ya Maendeleo 2050 na hatua za utekelezaji, sambamba na kujenga ushirikiano madhubuti ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia Watanzania wote.

Akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika jijini Arusha, CPA Mercy Sila, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Foundation for Civil Society (FCS) na Rais wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), alisema kuwa FCS inatamani kuona Tanzania yenye wananchi waliowezeshwa, wenye ustahimilivu, uwajibikaji na wanaopata haki zao za kijamii na kiuchumi, pamoja na maisha bora.

CPA Sila alieleza kuwa Wiki ya AZAKI inachangia moja kwa moja katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania kwa kuhamasisha ushiriki jumuishi na ushirikiano wenye tija, na hadi sasa, FCS imewezesha zaidi ya asasi 6,000 za kiraia kote nchini.

“Tukiwa kwenye maadhimisho haya ambayo ni ya saba tangu kuanzishwa, tunaendelea kuamini kuwa changamoto za kimfumo zinaweza kutatuliwa kupitia hatua za pamoja za wadau kutoka sekta mbalimbali,” alisema CPA Sila.

Justice Rutenge, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), alieleza kuwa na shauku kubwa juu ya majadiliano yanayotarajiwa kufanyika kuhusu Dira ya Maendeleo 2050, akisisitiza kwamba asasi za kiraia zimeshirikia kikamilifu na kutoa mchango kupitia majadiliano na taasisi za serikali.

“Majadiliano katika Wiki ya AZAKI kwa mwaka huu yataangazia nafasi ya utamaduni na rasilimali watu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050. Tutachambua namna ambavyo maadili, elimu, ujuzi na utambulisho wa kitaifa vinavyoweza kuathiri mwenendo wa maendeleo ya nchi kwa muda mrefu; sambamba na uwekezaji na ushirikiano unaohitajika ili kujenga taifa lenye watu wenye uwezo, maadili na uthubutu wa kusukuma gurudumu la maendeleo jumuishi na endelevu,” alisema Rutenge.

Naye Ismail Biro, Naibu Mkurugenzi wa Tanzania Bora na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi, alizungumzia umuhimu wa ushirikiano katika kuendeleza maendeleo jumuishi. Akihitimisha ujumbe wake kwenye mkutano na wanahabari, Biro alielezea jinsi wadau mbalimbali walivyoshirikiana kusaidia vijana wengi zaidi kushiriki katika wiki ya AZAKI 2025 baada ya programu ya Vodacom Young Changemakers kupokea idadi kubwa ya maombi.

“Tulifikisha taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Maandalizi na wadau wengine ili kuona namna wanavyoweza kutusaidia kuwawezesha vijana wengi zaidi kushiriki katika maadhimisho haya. Asasi ya Wajibika, kupitia ufadhili kutoka kwa FCDO na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, ilijitolea kufadhili ushiriki wa vijana 13 wenye ulemavu. Vilevile, mshirika wetu muhimu, MS TCDC, amedhamini gharama za malazi ya vijana 60,” alisema Bwn. Biro na pia kuitangaza Benki ya NMB kama mshirika mpya wa Wiki ya AZAKI 2025.

Kwa upande wake, Sandra Oswald, Meneja Mahusiano kutoka Vodacom Tanzania Foundation (VTF), alielezea ari yao ya kushirikiana na Wiki ya AZAKI kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo wamewezesha mradi wa vijana uitwao “Vodacom Youth Changemakers” unaotoa fursa kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini kushiriki kwenye maadhimisho haya.
“Katika kipindi cha miaka miwili ya ushirikiano wetu na Wiki ya AZAKI, tumeshuhudia hamasa kubwa waliyonayo vijana wa Kitanzania katika kutatua changamoto za jamii, na katika kushiriki kwenye mijadala kuhusu mustakabali wao. Mwaka huu, kupitia mradi wa Youth Changemakers, tumewawezesha vijana 100 kushiriki kwenye Wiki ya AZAKI 2025. Ushiriki wa vijana katika mijadala ya ngazi ya kitaifa kama Wiki ya AZAKI ni muhimu katika kujenga maendeleo jumuishi,” alisema Sandra.
Sandra aliongeza kuwa nguzo kuu za kimkakati za VTF ni kuwawezesha watu, kulinda mazingira na kuendeleza uaminifu. Uwezeshaji wa watu unahusisha mjumuisho wa kidijitali na kifedha, ujuzi, maendeleo, na mjumuisho kwa wote.

Wiki hii haijabaki ndani ya kumbi za mikutano pekee, bali itawafikia wananchi moja kwa moja. Washiriki watapata fursa ya kujifunza na kushiriki kwa pamoja na jamii. Baadhi ya shughuli za kijamii ni pamoja na mafunzo ya utayari wa kidijitali na kifedha (Digital & Financial Readiness Bootcamp) kwa wanawake wajasiriamali 200 yatakayoendeshwa na Vodacom Foundation.
Dickson Senzi, Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Stanbic Bank Tanzania, alisema kuwa benki hiyo imeandaa ziara itakayowawezesha washiriki kujionea mbinu za ushirikishwaji wa jamii katika elimu na mifumo jumuishi ya kifedha huko Karatu, pamoja na FinCafe itakayofanyika katika Wiki ya AZAKI 2025 katika Hoteli ya Mount Meru, ambapo AZAKI zitapewa ushauri wa kifedha ili kuwajengea uendelevu wa kifedha.

Wiki ya AZAKI 2025 inafadhiliwa na mashirika mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU), Ford Foundation, Wilde Ganzen, TradeMark Africa, Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na GIZ.



Prev Post Mashabiki Wa PSG Waunga Mkono Palestina Katika Mechi Ya Fainali Ya Klabu Bingwa Ulaya
Next Post Rihanna Afiwa Na Baba Yake Mzazi ‘Ronald Fenty’.
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook