

Dodoma, 30 Mei 2025 – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha maandalizi ya Ilani yake mpya ya Uchaguzi kwa mwaka 2025, ambayo imewasilishwa rasmi leo Mei 30, 2025 katika Mkutano Mkuu wa chama hicho unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Ilani hiyo mpya inajumuisha kurasa 78 zenye jumla ya maneno 29,520, na imeandaliwa kwa kushirikisha wataalamu wa kada mbalimbali, sambamba na maoni ya wananchi kutoka mikoa yote ya Tanzania. Hii ni ishara ya dhamira ya CCM ya kuendelea kujibu kwa vitendo mahitaji na matarajio ya Watanzania kwa miaka ijayo.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha muhtasari wa Ilani hiyo, Profesa Kitila Mkumbo alieleza kuwa maandalizi ya nyaraka hiyo yamezingatia kwa makini changamoto za sasa, fursa zilizopo, pamoja na matarajio ya Taifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
VIPAUMBELE TISA (9) VYA ILANI YA CCM 2025–2030
-
Kuchochea Mapinduzi ya Uchumi wa Kisasa
Kuendeleza sekta za viwanda, biashara, TEHAMA na huduma za kifedha ili kukuza uchumi shindani na jumuishi. -
Kuongeza Fursa za Ajira kwa Vijana na Kupunguza Umaskini
Kuweka mazingira wezeshi kwa ujasiriamali, mafunzo ya stadi za kazi, na uwekezaji katika sekta zenye ajira nyingi. -
Kuboresha Maisha ya Watu na Ustawi wa Jamii
Uboreshaji wa huduma za afya, elimu, maji safi na salama, pamoja na hifadhi ya jamii kwa makundi maalum. -
Kuimarisha Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji
Ujenzi wa barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege kwa ufanisi wa uchumi na kuunganisha mikoa. -
Kukuza na Kuimarisha Matumizi ya Sayansi na Teknolojia
Uwekezaji katika tafiti, uvumbuzi na TEHAMA ili kuharakisha maendeleo na ushindani wa kidijitali. -
Kudumisha Demokrasia, Utawala Bora na Uwajibikaji
Kuweka msisitizo kwa uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, utawala wa sheria, na kupambana na rushwa. -
Kuendelea Kudumisha Amani, Utulivu na Usalama wa Taifa
Kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, usimamizi wa mipaka, na udhibiti wa uhalifu wa mtandaoni. -
Kudumisha Utamaduni wa Kitaifa na Kukuza Sanaa na Michezo
Kukuza vipaji vya vijana, kuhifadhi turathi za taifa, na kuimarisha sekta za sanaa na burudani. -
Kuongeza Kasi ya Maendeleo Vijijini
Kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi vijijini ili kupunguza pengo la maendeleo kati ya vijijini na mijini.
MAKUSUDIO YA ILANI
Ilani hii inakusudia kuwa nyenzo ya mwelekeo wa maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha 2025 hadi 2030. Inalenga kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya nyuma, huku ikifungua njia mpya kwa mageuzi ya kijamii na kiuchumi yatakayowanufaisha Watanzania wote.
“Ilani hii imeandaliwa kwa makini kwa kuzingatia changamoto za sasa, fursa zilizopo, na matarajio ya Watanzania kwa miaka ijayo,”
— Prof. Kitila Mkumbo, 30 Mei 2025, Dodoma

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!