Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

BOT YASHINDA TUZO YA UBUNIFU HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA DUNIANI 

  • 4
Scroll Down To Discover

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Lucy Shaidi (kushoto), akiwa na Meneja Uhusiano wa BoT, Bi. Vicky Msina, wakishika Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) iliyotolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion – AFI), katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, Septemba 16, 2025, katika Ofisi za Benki hiyo jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Lucy Shaidi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) iliyotolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion – AFI)

Meneja Uhusiano wa BoT, Bi. Vicky Msina akizungumzia na waandishi wa habari kuhusu muhimu wa Tuzo hiyo.

Mutashobya Mushumbuzi Meneja Msaidizi, Kurugenzi Mifumo ya Malipo ya Taifa akiwa katika mkutano na waandishi wa habari.

Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) iliyotolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion – AFI).

………..

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kupata Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award) kutokana na utekelezaji madhubuti wa mifumo ya malipo ya kisasa, hatua ambayo imechangia kupunguza gharama za kufanya miamala kwa wananchi pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kifedha nchini.

Tuzo hiyo imetolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion – AFI), ambayo ina wanachama kutoka benki kuu na taasisi nyingine za udhibiti wa kifedha kutoka nchi 84 zinazoendelea duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa, Bi. Lucy Shaidi, amesema moja ya mafanikio makubwa yaliyoiweka Benki Kuu katika nafasi hii ni Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo unaojulikana kama Tanzania Instant Payment System (TIPS).

Bi. Shaidi amesema kuwa mfumo huo umeongeza urahisi wa kufanya miamala ya kifedha baina ya benki na watoa huduma wa kifedha wa kidijitali kwa wakati halisi, hivyo kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.

“Mafanikio mengine yametokana na matumizi ya msimbo milia wa malipo (QR Code) unaojulikana kama TANQR, ambao umeanzishwa ili kuwezesha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupokea malipo kwa urahisi kupitia simu au benki,” amesema Bi. Shaidi.

Ameongeza kuwa mchango wa Benki Kuu kwenye ubunifu huu umeonekana katika machapisho mbalimbali duniani kuhusu mifumo ya TIPS na TANQR. Aidha, Benki Kuu imekuwa mstari wa mbele katika kugawa ujuzi kwa nchi nyingine zinazojihusisha na ubunifu huu, ikiwemo Kenya, Lesotho, Rwanda, na Uganda.

Bi. Shaidi amefafanua kuwa mafanikio haya ya ubunifu yamechangia ongezeko kubwa la miamala kwa mwaka wa fedha 2024/25 kufikia milioni 560 zenye thamani ya takribani shilingi trilioni 41.

Kupitia maboresho haya ya teknolojia ya malipo, Benki Kuu inaendelea kuonesha dhamira ya kukuza uchumi wa kidijitali na kuhakikisha huduma rasmi za kifedha zinawafikia wananchi wengi.

“Tuzo hii mashuhuri inalenga kutambua nchi wanachama wa AFI ambazo zimeonesha juhudi kubwa katika ubunifu na matumizi ya teknolojia, pamoja na kutambua uongozi imara katika kuchochea kasi ya upatikanaji na matumizi ya Huduma Jumuishi za Fedha. Tanzania ni mwanachama wa taasisi hii kupitia Benki Kuu kuanzia mwaka 2011,” amefafanua Bi. Shaidi.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana anayeshughulikia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma Jumuishi za Fedha uliofanyika mjini Swakopmund, Namibia mwanzo wa mwezi Septemba 2025.

Katika hatua nyingine za kuchangia matumizi ya huduma jumuishi za fedha, Bi. Shaidi amesema Benki Kuu imeanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu kupitia Bank of Tanzania Fintech Regulatory Sandbox Regulations, 2024, ili kuchochea wabunifu kujaribu bunifu zao.

Pia, kwa kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wananchi, Benki Kuu imeanzisha mfumo maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi (SEMA na BoT), ili kuhakikisha kero zinazohusu huduma za fedha zinashughulikiwa kwa wakati.

Mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi thabiti wa Benki Kuu chini ya Gavana Emmanuel Tutuba katika kusimamia juhudi za kuongeza na kuchochea matumizi ya huduma za fedha kwa kutumia teknolojia.

“Hatua hizi zinalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama, na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa na kuboresha maisha yao,” amesema Bi. Shaidi.



Prev Post Wasichana Zaidi Ya 3370 Wanufaika Na Programu Ya Kompyuta Code Like A Girl
Next Post MARA YA SITA MFULULIZO….KICHWA KIMEPIGWA KOOO….PACOME AWAULIZA MASWALI MAGUMU …
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook