VIGOGO vya soka nchini, Simba, Yanga na Azam FC wamelainishwa mambo katika ishu za usajili, lakini wakabanwa kwa upande mwingine katika Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa msimu mpya wa 2025-26.
Msimu huo unatarajiwa kuzinduliwa na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16 Kwa Mkapa ikizikutanisha Simba na Yanga kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Septemba 17 kwa mechi mbili, KMC itakayovaana na Dodoma Jiji na Coastal Union itakayoialika Tanzania Prisons.
Kubanwa na kulainishiwa kwa vigogo hivyo na klabu nyingine za soka nchini kumetokana na mabadiliko ya kanuni za Ligi Kuu zilizotangazwa na Bodi ya Ligi (TPLB), ambayo imeridhia nyota 12 wa kigeni waliosajiliwa na klabu hizo kutumika kwa pamoja katika mechi moja ya Ligi na za FA.
Awali, kanuni ilikuwa ikizibana klabu kwa kutakiwa kuwatumia wachezaji wa kigeni wasiozidi wanane kati ya 12 waliosajiliwa kutumika katika mechi moja, lakini mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni yametoa wigo kwa klabu kuwatumia kwa mpigo bila tatizo.
Hata hivyo, klabu zimepigwa pini kusajili kipa wa kigeni zaidi ya mmoja kwa lengo la kulinda vipaji vya ndani katika mabadiliko hayo ya kanuni mpya za Ligi Kuu 2025-26 inayotarajiwa kuanza katikati ya mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPLB, Ibrahim Mwanyela, kanuni zilizofanyiwa marekebisho na kupitishwa katika kikao hicho ni pamoja na kanuni ya nane kuhusu mshindi, kanuni ya 11 kuhusu vikombe na tuzo, kanuni ya 17 kuhusu taratibu za mchezo, kanuni 57 kuhusu meneja wa mchezo na kanuni 62 kuhusu wachezaji wa kigeni.
Taarifa hiyo inasema kwenye kanuni ya 62 (1) klabu zinaruhusiwa kusajili wachezaji 12 wa kigeni kutoka sehemu yoyote duniani (mazingatio kwa kanuni 62:4 ya kanuni hizi).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kanuni 62 1.1 klabu inaweza kuwachezesha (kuwemo kwenye orodha ya wachezaji wa mchezo kwa siku husika) wachezaji wake wote 12 wa kigeni katika mchezo mmoja wa ligi au Kombe la Shirikisho.
Wakati huo huo, kanuni hizo zimezibana Simba, Yanga, Azam FC, Singida Black Stars, Namungo na nyingine zote kusajili makipa zaidi ya wawili wa kigeni msimu ujao 2025-26, kwani awali kanuni hii ilikuwa haiwabani, hivyo klabu hizo zenye uwezo wa kusajili zitakavyo kubeba zaidi ya kipa mmoja.
Katika hatua nyingine mabadiliko hayo kanuni ya 41:2 (2.3) udhibiti wa wachezaji awali ilikuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata, lakini kwa sasa mchezaji atakayeonyeshwa kadi nne za njano ndio hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata.
MAREFA KUTOKA NJE
Kanuni ya 39 inayowahusu waamuzi, kipengele cha (7) kamati ya waamuzi ya TFF itapanga waamuzi katika michezo ya Ligi Kuu na ndio pekee yenye mamlaka ya kupanga, kubadilisha na kuondoa mwamuzi kwenye ratiba kwa utaratibu na mfumo uliowekwa, kwa kushirikiana na Sekretarieti ya TFF kwa mazingira ya kanuni.
Kanuni mpya ya (7) Kamati ya Waamuzi ya TFF itapanga waamuzi kwenye michezo ya Ligi Kuu na ndiyo pekee yenye mamlaka ya kupanga, kubadilisha na kuondoa mwamuzi kwenye ratiba kwa Utaratibu na mfumo uliowekwa (kwa kushirikiana na Sekretarieti ya TFF) kwa Mazingatio ya Kanuni hizi.
Kanuni ya (7.1): Kamati ya Waamuzi ya TFF inaweza kupanga Waamuzi kutoka nje ya Tanzania kwenye Michezo ya Ligi.
Kanuni ya 45 udhibiti wa makocha ndivyo ilivyokuwa inatambulika awali sasa jina la kanuni ya uthibiti wa makocha limebadilishwa na sasa linasomeka udhibiti wa makocha na maofisa wengine wa ufundi.
The post KANUNI MPYA TFF….SIMBA, YANGA KUCHEZESHWA NA REFA KUTOKA NNJE…MAPRO WOTE RUKSA… appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!