
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) Kanda ya Serengeti, Resemary Kirigini, amejiunga rasmi na Chama cha ACT Wazalendo.
Kirigini, ambaye pia amewahi kuwa Mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushika nyadhifa za Mkuu wa Wilaya za Meatu na Maswa, alitangaza uamuzi huo Jumamosi Agosti 16, 2025, wakati wa mkutano wa mapokezi ya mgombea urais wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, uliofanyika Jimbo la Kisesa.

Akizungumza baada ya kupokelewa, Kirigini alisema amejiunga ACT Wazalendo kwa imani kuwa chama hicho kitaleta mabadiliko ya kweli nchini na kusisitiza dhamira yake ya kushirikiana na viongozi na wanachama wenzake kuhakikisha chama kinapata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kwa upande wake, mgombea urais wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, alimkaribisha Kirigini na kueleza kuwa uamuzi huo ni nguvu mpya kwa chama kuelekea kampeni za kitaifa.
Kujiunga kwa Kirigini kunatajwa kuwa ni hatua muhimu kwa ACT Wazalendo katika mkakati wake wa kuvutia wanachama wapya na kuimarisha mtandao wa kisiasa hasa katika maeneo ya Kanda ya Serengeti na mikoa jirani.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!