KWA wasiojua ni Jumamosi ya Oktoba 5, 2024, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alitakiwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na Azam FC.
Mkataba huo ulikuwa ukiunganisha na ule aliokuwa nao awali baada ya kuondoka Yanga kitatanishi hadi kusababisha Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati alipoialika klabu hiyo Ikulu kuwapongeza kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023.
Inaelezwa makubaliano yalishafikiwa na upande wa mchezaji ukapewa nakala ya mkataba iupitie kifungu kwa kifungu kabla ya kusaini.
Hayo yalifanyika takriban wiki moja kabla ya siku ya tukio.
Ilipofika siku hiyo, uongozi wa Azam ukafika eneo la tukio yaani pale Mzizima, ukimsubiri Fei Toto na watu wake, kumaliza jambo.
Wakati huo timu ya taifa, Taifa Stars, ilikuwa imeitwa kujiandaa na mechi ya kufuzu AFCON 2025 ugenini dhidi ya DR Congo.
Fei Toto alitakiwa atoke kwenye kambi ya timu hiyo ya taifa, akasaini mkataba halafu arudi kambini, kwani Jumanne ya Oktoba 8 timu ilikuwa ikitakiwa isafiri kwenda Kinshasa kwa mechi ya Oktoba 10.
Hii ndio ile mechi ambayo Stars ilipoteza 1-0 kwa bao la kujifunga la Clement ‘Waleed’ Mzize.
Viongozi wa Azam wakafika Mzizima, makao makuu ya klabu, wakimsubiri Fei Toto na watu wake wafike…wakasubiri…subiri… subiri na wewe.
Baadaye ikaja taarifa Fei Toto na watu wake wameshindwa kufika kwa sababu mwanasheria alikuwa hajamaliza kuupitia mkataba, hivyo tukio liahirishwe hadi wakati mwingine mchezaji atakaporudi kutoka Kinshasa.
Tangu Oktoba 2024 hadi Julai 2025 ni miezi 10….Fei Toto bado hajasaini mkataba mpya na Azam.
Sio kwamba mwanasheria wake hajamaliza kusoma mkataba…bali upande wa mchezaji umekuwa na danadana nyingi sana.
Siku nyingine tutazihesabu danadana hizo, lakini leo nataka kuzungumzia hasara ambayo Fei Toto ameipata hadi sasa kwa kushindwa kwake kusaini mkataba huo.
MKATABA WENYEWE
Azam ilimwekea Fei Toto mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya takribani Sh2 bilioni.
Ada ya kusainia mkataba ilikuwa Dola 200,000 kwa mwaka…ikiwa na maana kwa miaka miwili kiungo huyo angevuta Dola 400,000 (zaidi ya Sh1 Bilioni) na mshahara wa Sh80 milioni kwa mwezi kabla ya kodi…baada ya kodi ni Sh50 milioni. Pia alipewa mikataba mingine ya ubalozi wa bidhaa za kampuni…yenye thamani ya Sh5 milioni kwa mwezi.
HASARA
1. Ada ya kusainia mkataba
Angesaini mkataba siku ile, angepata Sh1 Bilioni…kwa kuwa hakusaini, hajaipata.
2. Mshahara
Angesaini mkataba siku ile, angepata mshahara wa Sh50 milioni kwa mwezi na wa sasa ni Sh15 milioni kwa mwezi.
Maana yake amepoteza Sh35 milioni kwa mwezi na kwa miezi 10 ni Sh350 milioni. Yaani kwa kutosaini tu siku ile, amejipotezea Sh350 milioni hadi sasa.
3. Mafao
Azam huwalipia mafao wachezaji wake, tofauti na klabu nyingine, utaratibu ambao mshahara wa jumla wa mchezaji unakatwa asilimia 10 na mwajiri anaweka asilimia 10.
Endapo angesaini, mshahara wa jumla ungekuwa Sh80 milioni.
Asilimia 10 yake ni Sh8 milioni na mwajiri angeweka Sh8 milioni…maana yake kwa mwezi angekuwa anawekewa Sh16 milioni. Kwa miezi 10 ambayo imepita tangu akwepe kusaini, angekuwa amewekewa Sh160 milioni.
4. Mkataba wa ubalozi.
Alipewa ofa ya ubalozi wa bidhaa za Azam ambao ungemuingizia Sh5 milioni kwa mwezi. Kwa miezi 10 ingekuwa Sh50 milioni hadi sasa.
Jumla
Ada ya kusiania mkataba – 1,042,314,800./=
Mshahara – 350,000,000/=
Mafao – 160,000,000/=
Ubalozi – 50,000 000/=
Jumla = 1,602,314,800/=
Hii ina maana Fei Toto amepoteza Shilingi bilioni moja, milioni mia sita na ushei kwa miezi 10 hadi sasa kwa kutosaini mkataba ule wa Oktoba mwaka jana.
Na inavyoonekana hataki kusaini mkataba mpya ili amalize uliopo na aondoke zake.
Kwa kufanya hivyo, atakuwa amepoteza fedha nyingi zaidi ya hizo kwa sababu bado ana mwaka mzima mbele.
Je, huko atakakoenda atasaini mkataba utakaofidia pesa yote hii ambayo ameipoteza hadi sasa?
Au endapo akiamua kusaini mkataba mpya na Azam sasa, atairudishaje pesa yote hii iliyomwagikia chini kwa kushindwa kwake kusaini siku ile?
Fei Toto ana washauri wabaya au vile ana ndoto yenye thamani kubwa zaidi ya kiasi hiki alichokipoteza? Majibu atakuwa anayo mwenyewe!
C&P From MwanaSpoti.
The post KISA DILI LAKE LA SIMBA….FEI TOTO APOTEZA TSH BIL 1.6 …, AKATAA MSHAHARA WA MIL 80 AZAM FC… appeared first on Soka La Bongo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!