
Hayati Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora, na ustawi wa Taifa.
Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliweka nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani, na mshikamano wa Watanzania, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika bara la Afrika na ulimwenguni.
Nimeyasema hayo nilipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya Miaka Mitano ya Hayati Benjamin William Mkapa, iliyofanyika leo tarehe 23 Julai 2025, Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.
Hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi, lakini pia alihakikisha kuwa maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
Aidha, Mzee Mkapa ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu katika mageuzi ya maendeleo, na mafanikio yake yamekuwa msingi wa kuzinduliwa kwa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Nilipata fursa ya kuzuru kaburi la Hayati Mzee Mkapa na kuweka shada la maua, nikiwa pamoja na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi na mkewe, pamoja na Mjane wa Hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!