

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, amefanya uteuzi mkubwa kwa kumteua Dkt. Justin Nsengiyumva kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo, akichukua nafasi ya Dkt. Edouard Ngirente aliyehudumu tangu mwaka 2017.
Uteuzi huu umetangazwa rasmi Julai 24, 2025, na unakuja katika kipindi ambacho Rwanda inaendelea kusukuma mbele ajenda zake za maendeleo na mageuzi ya kiuchumi.
Wasifu wa Dkt. Nsengiyumva
Kabla ya uteuzi wake, Dkt. Justin Nsengiyumva alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Rwanda (BNR), wadhifa aliouteuliwa Februari 25, 2025. Katika nafasi hiyo, alisimamia sera za kifedha na udhibiti wa mfumo wa benki nchini.
Dkt. Nsengiyumva pia ni mtaalamu mahiri wa uchumi mwenye uzoefu mpana serikalini:
Aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu hadi mwaka 2008,
Baadaye akahudumu kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, akishiriki kikamilifu katika sera za kukuza viwanda na uwekezaji nchini Rwanda.
Amehitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza, na anajulikana kwa mchango wake mkubwa katika sera za uchumi na maendeleo ya taifa.
Anamrithi Nani?
Dkt. Edouard Ngirente, ambaye Dkt. Nsengiyumva anamrithi, aliongoza serikali ya Rwanda kwa takribani miaka minane. Wakati wake madarakani ulitawaliwa na jitihada za kuimarisha sekta za elimu, afya, teknolojia na diplomasia ya kikanda.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!