Rais wa Kenya, William Ruto amewataka wapinzani wake kueleza mipango yao mbadala ya kutengeneza ajira kwa vijana badala ya kuwachochea vijana kufanya fujo na kuharibu mali.
Rais Ruto amesema ana mpango madhubuti ambao tayari unazalisha maelfu ya ajira kwa vijana, tofauti na wapinzani wake ambao, kwa mujibu wake, hawana mpango wowote.
Ameeleza kuwa mpango wa Climate WorX umezalisha ajira 200,000 nchi nzima, wakati zaidi ya 320,000 wanafanya kazi kupitia mradi wa Nyumba Nafuu, na idadi hiyo itazidishwa mara mbili ndani ya miezi mitatu ijayo.
Ruto ameeleza kuwa tayari watu 400,000 wamepata ajira kupitia mpango wa ajira nje ya nchi, na wengine 180,000 wameajiriwa katika kazi za kidijitali.
“Mpango wenu ni upi? Huwezi kusema mpango wako ni kuwalipa vijana wachome mali na kufanya vurugu. Hiyo haikubaliki,” amesema Rais Ruto.
Aidha, Rais Ruto amesisitiza kuwa anajitahidi kuunganisha Wakenya wote na kuondoa ukabila na migawanyiko, akisisitiza kuwa mazingira ya vurugu hayawezi kusaidia maendeleo ya taifa wala uundaji wa ajira.
The post Ruto: Wapinzani hawana mipango ya ajira, wanachochea vurugu appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!