
Nairobi, Kenya – Rais William Ruto ametangaza rasmi uteuzi mpya wa Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kipindi cha miaka sita, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ulioidhinisha uhalali wa mchakato huo.
Kupitia Gazeti Rasmi la Serikali nambari 9269, lililotolewa Julai 10, 2025, Rais Ruto alimteua Erastus Edung Ethekon kuwa Mwenyekiti mpya wa IEBC, akichukua nafasi hiyo kwa muhula wa miaka sita.
Katika tangazo tofauti, kupitia Gazeti la Serikali nambari 9270, Ruto pia aliwateua watu sita kuwa makamishna wa IEBC kwa kipindi sawa cha miaka sita. Wateule hao ni:
Ann Njeri Nderitu
Moses Alutalala Mukhwana
Mary Karen Sorobit
Hassan Noor Hassan
Francis Odhiambo Aduol
Fahima Araphat Abdallah
Uteuzi huo umekuja baada ya Mahakama Kuu, kupitia majaji watatu, kutupilia mbali ombi la kupinga uteuzi huo, lililowasilishwa na walalamikaji waliodai kuwa uteuzi huo ulikuwa na dosari za kikatiba na kisheria.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa ilani ya awali ya Gazeti iliyokuwa imetolewa awali na Rais ilichapishwa kwa kukiuka agizo la mahakama, na hivyo ikaamuru kuchapishwa upya kwa notisi hizo. Kwa mujibu wa uamuzi huo, uteuzi wenyewe ulibakia kuwa halali.
Kwa sasa, Mwenyekiti na Makamishna walioteuliwa wanatarajiwa kula kiapo mbele ya Jaji Mkuu, kabla ya kuanza rasmi majukumu yao katika usimamizi wa uchaguzi na mipaka nchini.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!