MAGAZETI ya Leo Jumamosi 14 June 2025
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mnguto, amewasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake, hatua inayokuja wakati ambapo kumekuwepo na mijadala mingi kuhusu mwenendo wa uendeshaji wa ligi hiyo.
Taarifa ya kujiuzulu kwa Mnguto imethibitishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), likieleza kuwa barua hiyo imepokelewa rasmi na uamuzi huo utazingatiwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za shirikisho hilo.
Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Wallace Karia, amemsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo, hadi hapo uchunguzi dhidi yake utakapokamilika. Taarifa ya TFF iliyotolewa usiku huu na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao, haijaeleza sababu rasmi ya kusimamishwa kwa Kasongo, lakini imesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa kiutawala unaolenga kuboresha uendeshaji wa ligi.
Hatua hizi mbili zimekuja wakati kukiwa na mvutano wa mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba ambayo awali ilikuwa ipigwe Machi 8, mwaka huu kabla ya kusogezwa mbele hadi Juni 15 mwaka huu. Hata hivyo wakati kukiwa na mvutano huo huku kila timu ikivutia upande wake bodi ya ligi imetangaza kuwa mchezo huo sasa utapigwa Juni 25.
Ratiba hiyo mpya ya mchezo namba 184 imekuja kufuatia viongozi waandamizi wa timu hizo kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dodoma mapema leo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!