
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa kuna kila sababu ya kushinda Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa Ilani ya CCM imetekelezwa kikamilifu kwa vitendo.
Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati akizindua rasmi Tawi jipya la Chama Cha Mapinduzi (CCM) lililopo Mpendae Juu, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 17 Mei 2025.
Aidha, amewapongeza wana-CCM kwa kazi nzuri waliyoifanya katika zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu na kuwataka kujitokeza kwa wingi wakati wa Uchaguzi ili kupata ushindi wa wa kishindo.
Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa kila mwanachama aliyejiandikisha ana wajibu wa kupiga kura, na kwamba ni muhimu kuhakikisha hakuna anayekosa kutekeleza jukumu hilo muhimu.
Ameeleza kuwa CCM ina dhamira ya dhati ya kuendelea kushika Dola na kutekeleza maendeleo makubwa zaidi, hivyo ushindi wa CCM ni jambo lisiloepukika.
Katika hatua nyingine, amewapongeza viongozi wa Jimbo la Mpendae kwa juhudi walizozionesha katika ujenzi wa tawi hilo jipya lenye hadhi ya CCM.
Tawi hilo limejengwa kwa ushirikiano kati ya Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Mhe. Toufiq Salim Turky, na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Shaaban Ali Othman likiwa na Afisi za Jumuiya zote za CCM, Ukumbi wa Mikutano, Ukumbi wa Sherehe, maduka pamoja na vyoo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!