Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

BENKI YA STANBIC YASHIRIKIANA NA VIONGOZI WA RASILIMALI WATU KUBORESHA USTAWI WA KIFEDHA KWA WAFANYAKAZI

  • 11
Scroll Down To Discover

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Benki ya Stanbic Tanzania imeweka ustawi wa kifedha wa wafanyakazi kama kichocheo cha tija kazini, baada ya kuwakutanisha viongozi wa rasilimali watu kutoka mashirika mbalimbali katika hafla ya HR Summit Dinner iliyofanyika Ijumaa, 19 Septemba 2025, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya benki hiyo, ililenga kujadili namna ya kupunguza msongo wa kifedha miongoni mwa wafanyakazi ili kuongeza uaminifu, utulivu na utendaji bora kazini. Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa “Kuwawezesha wanaowawezesha wafanyakazi.”

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Huduma za Wateja Binafsi wa Stanbic, Bw. Omari Mtiga, alisisitiza uhusiano wa moja kwa moja kati ya usalama wa kifedha wa mfanyakazi na tija kazini.

 “Wafanyakazi wanapokuwa salama kifedha, hufanya kazi kwa bidii, huonyesha uaminifu na ubunifu zaidi. Kwa Stanbic, tunaona viongozi wa HR kama washirika muhimu katika kujenga taasisi zenye wafanyakazi wanaostawi,” alisema.

Kilele cha hafla hiyo kilikuwa ni uwasilishaji wa huduma za Employee Value Banking (EVB) uliofanywa na Bw. Emmanuel Mahodanga, Mkuu wa Huduma za Benki Watu Binafsi, na Bw. Priscus Kavishe, Meneja Mwandamizi wa Mauzo na Uajiri. Programu hiyo inatoa huduma mahsusi za kifedha zinazolenga kuwasaidia wafanyakazi kulipa madeni, kupanga maisha ya uzeeni na kukuza akiba.

Aidha, mijadala ya Financial Fitness at Work iliyoendeshwa na Bw. Elibariki Ndossi, Mkuu wa Uwekezaji, pamoja na Bi. Janeth Mosha, Afisa Uwekezaji, ilijadili nafasi ya idara za HR katika kuingiza ustawi wa kifedha kwenye mipango ya wafanyakazi. Masuala ya msongo wa madeni, maandalizi ya maisha ya uzeeni na mapengo ya akiba yalijadiliwa sambamba na nyenzo za vitendo zinazoweza kutolewa na Stanbic moja kwa moja kwa wafanyakazi.

Washiriki pia walipokea mawaidha kutoka kwa Bw. Charles Nduku, huku baadhi ya wateja wakitoa ushuhuda juu ya namna huduma za kifedha za Stanbic zilivyosaidia kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na taasisi zao.

Akihitimisha hafla hiyo, Bw. Mahodanga alitoa mwito kwa viongozi wa HR kupanga vipindi maalum vya Financial Fitness kwa wafanyakazi wao, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na uthabiti wa rasilimali watu katika taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Stanbic, HR Summit Dinner haikuwa tu sehemu ya sherehe za kumbukizi ya miaka 30 ya benki hiyo, bali pia ni uthibitisho wa dhamira ya kuendelea kushirikiana na waajiri katika kujenga nguvu kazi yenye afya, thabiti na imara kifedha.



Prev Post TAKUKURU MWANGA YAFANIKISHA KUREJESHWA MILIONI 24.1 SERIKALINI
Next Post Md Twange Aridhishwa Na Maendeleo Ya Mradi Wa Taza – Aagiza Kuongezwa Kwa Kasi Ya Utekelezaji
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook