Na Neema Mtuka Sumbawanga
RUKWA : Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, amesema uzinduzi wa dawati Maalumu la uwezeshaji biashara ni hatua muhimu itakayowawezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa weledi na kuchangia ustawi wa Taifa.
Akizungumza leo Septemba 18,2025 katika viwanja vya ofisi ya (TRA) mkoa wa Rukwa wakati wa uzinduzi wa dawati hilo Nyerere amesema litawawezesha wafanyabiashara kulipa kodi wakiwa na uelewa zaidi.
Nyerere amesema dawati hilo litasaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kikodi kwa wakati pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili walipakodi.
“.Litumieni vyema dawati hili kwa manufaa ya shughuli zenu za kibiashara ikiwa ni Pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili kupitia dawati hili litawanufaisha”amesema Nyerere.
Nyerere amewataka wafanyabiashara wote mkoani humo kulitumia ipasavyo dawati hilo kwa manufaa ya shughuli zao, huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kusimama bega kwa bega nao katika kuhakikisha biashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Rukwa, Husna Nyange, amesema dawati hilo litakuwa daraja muhimu kati ya Serikali na wafanyabiashara kwa kusaidia kutoa taarifa sahihi na za haraka kuhusu masuala ya kodi pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Aidha Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara waliohudhuria uzinduzi huo akiwemo Martha Kataila ameipongeza (TRA) kwa hatua hiyo, akisema dawati hilo litaboresha zaidi mahusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara na kuwa chachu ya maendeleo ya biashara mkoani Rukwa.
“Dawati hili litaleta mahusiano mazuri kati ya serikali na wafanyabiashara na nina Imani tutaondokana na usumbufu na changamoto tunazozipata katika biashara zetu ikiwemo ulipaji wa kodi na kubambikiziwa kodi zisizo za lazima.”amesema Kataila.
Ujio wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara utawainua wafanyabiashara wengi na kuachana na mazoea ya kufanya biashara ya aina moja bila mafanikio.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!