
Dar es Salaam – Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh86 bilioni kupitia harambee ya kuchangia maandalizi ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na miradi ya maendeleo ya chama.
Harambee hiyo ilifanyika usiku wa Jumanne, Agosti 12, 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa chama, wafanyabiashara, wadau wa maendeleo na wanachama wa CCM kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kati ya fedha zilizopatikana, Sh56.3 bilioni ni fedha taslimu na Sh30 bilioni ni ahadi, huku akibainisha kuwa lengo la chama ni kufikia Sh100 bilioni kabla ya uchaguzi.
Akihutubia wageni waalikwa, Rais Samia aliwapongeza wote waliotoa michango, akisisitiza kuwa rasilimali hizo zitawezesha kufanikisha kampeni za chama kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025, na kuelekea siku ya uchaguzi mkuu itakayofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
“CCM imefanikisha mambo mengi kwa kutumia fedha zake, lakini tumeona waitishe harambee hii kuongeza nguvu. Tunaomba waendelee kuchangia, muda bado upo,” alisema Rais Samia.
Harambee hii imekuwa mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya kuchangisha fedha katika historia ya chama hicho, ikionesha mshikamano wa wanachama na wadau wake kuelekea ushindani wa kisiasa wa mwaka huu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!