Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

KISA YANGA KUWA NA THAMANI YA BIL 100….UTATA WAIBUKA…HOJA NZITO IKO HAPA….

  • 37
Scroll Down To Discover

HUKO mtandaoni na hata mitaani kwa sasa mjadala ulioteka wadau wa soka ni ishu ya thamani ya Sh100 bilioni iliyonayo Yanga baada ya kutangazwa katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa The Super Dome Masaki, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 627, Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji wa klabu hiyo, Alex Mgongolwa, alisema kwa sasa thamani ya timu hiyo imefikia kiasi cha Sh100 bilioni, jambo lililoibua maswali kwa wadau mbalimbali.

“Nichukue nafasi hii kuwaambia rasmi wanachama wa Yanga, thamani ya timu yetu imefikia Sh100 bilioni,” alisema Mgongolwa alipopewa nafasi na rais wa klabu hiyo kongwe nchini, Injinia Hersi Saidi kwa ajili ya kutoa ripoti ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.

Sababu ya thamani hiyo kugeuka gumzo imetokana na baadhi ya wadau kuhoji na kudai thamani hiyo ni kubwa kuliko baadhi ya vigogo vya soka Afrika ambao wapo katika orodha ya klabu zenye thamani kubwa kutokana na mali inazomiliki ikiwamo miundombinu na hata wingi wa mashabiki.

Pia wapo wengine wamekuwa wakiitilia shaka kutokana na ukweli kwa klabu kama Yanga isiyokuwa hata na uwanja wa mazoezi inawezaje kuwa na thamani hiyo? Na baadhi kuona ni kama kutaka kujimwambafai ili kuwakonga nyoyo watani wao ambao miaka michache iliyopita ilitoa tathamini ya klabu hiyo kuwa ina thamani ya Sh20 bilioni.

Hata hivyo, wapo watetezi wanaoamini thamani hiyo ni sahihi kwa Yanga kutokana na wingi wa mashabiki iliyonao, ukubwa wa nembo, udhamini ilionao na hata majengo inayoyamiliki, pia wakiamini huenda thamani hiyo ikawa ndogo kuliko iliyotangazwa, japo hofu yao waliofanya tathmini na kupata thamani hiyo ni kina nani na ilifanywa kwa vigezo vipi?

Maswali mengi kwa wadau wa soka nchini, yamejitokeza baada ya thamani hiyo kuonekana kubwa kuliko hata iliyonayo klabu ya Al Ahly ambayo ni Euro 30 milioni (sawa na Sh88 bilioni), ikiwa ni zaidi ya Sh12 bilioni ya ilizonazo kikosi hicho kwa orodha ya mwaka 2024.

Katika kuweka mambo sawa wachumi mbalimbali wametoa tathmini na mitazamo tofauti waliyonao katika suala hilo la thamani ya Sh100 bilioni ya klabu ya Yanga.

Mkuu wa Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora, aliliambia gazeti la Mwanaspoti, thamani ya taasisi au kampuni hupimwa kwa zaidi ya vitu vitatu, ambapo cha kwanza ni suala nzima la fedha inazoziingiza kutoka kwa wanachama au wawekezaji wake.

“Kampuni hata kama ikiwa na madeni huwa tunaihesabia imeongezeka thamani yake, magari, majengo, namba ya wanachama wake kwa maana wanavyochangia mapato na mengineyo, hivyo mnapojadili au kubisha inapaswa kuzingatia hayo,” alisema.

Aurelia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), alisema mbali na hilo, thamani nyingine inawezwa kupimwa kwa kuangalia endapo Yanga isipocheza michuano mbalimbali inaweza kuingiza hasara kiasi gani.

“Ninaposema Yanga isipocheza inaingiza hasara kiasi gani, hapa namaanisha ni vitu vingapi vitakuwa haviingizi mapato kwa mfano mashabiki watakuwa hawaingii uwanjani na mengineyo, hiyo ni ishara ya kupima thamani husika ya klabu au taasisi.”

Aidha, Profesa Aurelia alisema ilichokifanya Yanga ni mfano wa kuigwa kwa kuweka thamani kubwa tena ikiwa kwa mfumo wa fedha za Kitanzania, kwani itawafanya wawekezaji wanaowekeza kutambua wanapaswa kujipanga kutokana na kiwango hicho.

Profesa wa Uchumi, Semboja Haji alisema ili thamani ya taasisi au kampuni ionekane imeongeka kuna vitu vya kuangalia kwa mfano, benki wana kiasi gani, wana rasilimali za aina gani kwa maana ya viwanja, majengo na wanachama wao walionao.

“Viwango vya wachezaji ambao ikiwauza wanapata kiasi gani, klabu ikiwa na deni, je wanachama wana uwezo wa kulilipa, pia wanachama wana uwezo kwa kiwango gani, hivyo ni vitu ambavyo unaweza kuvipima na kutambua thamani ya kampuni,” alisema Semboja.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk Donald Mmari alisema ili uthaminishe thamani ya taasisi au kampuni ni lazima pia uangalie ina uwezo wa kuzalisha fedha kwa kiwango gani kwa muda fulani, ambao ukizidisha kwa miaka 10 unapata uhalisia.

“Sijui Yanga wametumia mfumo gani kujua thamani yao, ila ninachoweza kusema, unapoangalia suala hilo ni lazima uangalie hiyo kampuni au taasisi inaingiza kiasi gani, ambazo ukilinganisha miaka mitano au 10 unapata thamani halisi ya leo.”

Mwandishi wa Habari za Fedha na Mshauri wa Masuala ya Habari wa Gazeti la The Citizen, Samuel Kamndaya alisema Thamani Halisi ya Mali (Net Asset Value (NAV) ya kampuni ni jumla ya mali zake ukipunguza madeni yote na mara nyingi huonyeshwa kwa kila hisa au kipimo maalum. “Hii inaonyesha thamani halisi ya kampuni, mfuko wa uwekezaji au taasisi, na kuwawezesha wawekezaji kupima thamani ya hisa zao na kufuatilia mwenendo wa uwekezaji kwa muda. Ukweli ni kwamba Yanga ina baadhi ya mali, zikiwamo jengo la makao makuu na ardhi katika eneo la Jangwani. Yanga pia ina wachezaji wenye thamani ya soko, pamoja na wadhamini na washirika wa kibiashara ambao pia ni sehemu ya NAV ya klabu,” alisema Kamndaya kupitia andiko lake na kuongeza; “La msingi zaidi, wachambuzi hao walishindwa kuelewa ni kwamba kwa klabu iliyo imara kama Yanga, thamani yake halisi ni kubwa zaidi ya ile inayoonekana kwenye Taarifa ya Hesabu za Kampuni (Balance Sheet). Hapo ndipo kanuni ya Premium to NAV inapokuja.

“Thamani ya soko ya Yanga haitapimwa kwa NAV peke yake, bali kwa kuongezewa kiwango cha juu kutokana na uongozi wake imara, mikakati ya chapa (branding), mbinu za uwekezaji na matarajio chanya ya faida kwa siku za usoni.”

Anafafanua zaidi kwa kusema; “Premium to NAV ni hali ambayo hisa za mfuko wa uwekezaji zilizofungwa (closed-end fund) zinauzwa kwa bei ya juu kuliko thamani halisi ya mali zake. Tofauti hii hutokana na mtazamo chanya wa wawekezaji, mara nyingi ukichochewa na uongozi bora na mikakati endelevu.

Kimataifa, inakubalika kwamba kampuni zilizo na chapa thabiti mara nyingi hupata Premium to NAV kati ya mara mbili hadi tatu ya thamani iliyoko kwenye Balance Sheet.”

Pia aliongeza kwa kusema; “Hivyo maswali ya msingi ambayo mchambuzi yeyote makini anapaswa kuuliza ni: Je, Yanga ni klabu yenye chapa thabiti? Je, Yanga ni taasisi iliyo imara? Je, Yanga ina uongozi madhubuti? Je, kweli ni sahihi kudai kwamba hata kwa kipimo cha Premium to NAV thamani yake haiwezi kufikia Sh bilioni 100?”

Anafafanua kwa kusema; “Majibu ya maswali haya ndiyo yatakayoelekeza mjadala wa maana.

Kimsingi, uongozi wa Yanga umeonyesha kwamba huwezi kumvutia mwekezaji anayejielewa kama hujui thamani halisi ya kampuni yako.”

Hapa chini ni baadhi ya vigezo muhimu vya kutathmini thamani ya klabu za soka kwa mujibu wa mitandao.

MAPATO YA KLABU

(REVENUE)

– Mauzo ya tiketi za mechi (matchday revenue).

– Haki za matangazo ya televisheni.

– Mapato kutoka udhamini (sponsorship deals).

– Uuzaji wa jezi na bidhaa nyingine (merchandise).

MALI NA RASILIMALI (ASSETS):

– Viwanja na miundombinu (stadiums, training grounds).

– Vinginevyo kama akademi za vijana na wachezaji waliopo (player market value).

– Umaarufu na mashabiki (Fan base):

– Idadi ya mashabiki ndani ya nchi na kimataifa.

– Ufuatiliaji kwenye mitandao ya kijamii.

MAFANIKIO YA MASHINDANO:

– Makombe ya ndani na ya kimataifa.

– Ushiriki na mafanikio katika michuano mikubwa kama CAF Champions League.

– Uwekezaji na usimamizi (Management & Investment):

– Wamiliki wenye nguvu za kifedha.

– Uendeshaji bora wa kifedha (financial stability).

CREDIT::- MWANASPOTI

The post KISA YANGA KUWA NA THAMANI YA BIL 100….UTATA WAIBUKA…HOJA NZITO IKO HAPA…. appeared first on Soka La Bongo.



Prev Post KWA MAGORI, BARBARA NA MKWABI…SAPRIZI MPYA SIMBA HII HAPA…
Next Post ALIYETOKA LIGI ‘DARAJA LA KWANZA’ ATOA AHADI YA MAKOMBE SIMBA….
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook