Rais Samia Suluhu amesema kukamilika kwa kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya urani kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, ni hatua ya kimkakati itakayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 wakubwa zaidi wa urani duniani ikiwa ni rasilimali muhimu katika uzalishaji wa nishati safi.
Akizungumza mbele ya wananchi mara baada ya kuzindua kiwanda hicho, Rais Samia amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya serikali kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda unaojitegemea, huku akisisitiza kuwa kila hatua ya utekelezaji itazingatia viwango vya kimataifa, usalama wa afya na mazingira.
Ameeleza kuwa tayari ameshuhudia kwa macho mitambo ya uchenjuaji wa madini hayo na kupongeza namna mwekezaji alivyojipanga kuongeza thamani ya rasilimali hiyo ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mradi huo unatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 20 ya uzalishaji na katika kipindi hicho, ambapo Tanzania itanufaika kwa uwekezaji wa takriban dola za Marekani bilioni 1.2 [sawa na zaidi ya TZS trilioni 3.2], ajira zipatazo 3,500 hadi 4,000 wakati wa ujenzi wa miundombinu, ajira za moja kwa moja za kudumu zipatazo 750, na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 kutokana na shughuli zitakazochochewa na uwepo wa mradi huo.
The post Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji 10 wakubwa wa urani duniani appeared first on SwahiliTimes.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!