
Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), imetangaza kuanza mchakato wa kuwaondoa watoa huduma waliopo sasa kwenye Barabara Kuu za Mwendokasi jijini Dar es Salaam, zikiwemo Barabara ya Morogoro, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kwao kuongeza ufanisi, kutokuongeza mabasi kwa wakati na kutokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 24, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango mpya wa maboresho ya huduma za usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.
“Kwa lugha nyepesi, tumeanza sisi wenyewe kujisahihisha. Tulidhani wanatoa huduma vizuri na wana commitment, lakini tunaona hapana. Ni kama wanatufikia tu, na Watanzania wanaendelea kuteseka,” amesema Chalamila, akiashiria wazi kwamba kampuni ya UDART haitakuwa sehemu ya mpango mpya unaoanza.
Akizungumza akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athuman Kihamia, RC Chalamila amesema kuwa mabasi mapya yataanza kuingia barabarani hivi karibuni, na kwamba huduma zitaboreshwa kwa viwango tofauti, zikiwemo za kawaida na huduma ya VIP Class kwa abiria wanaotaka kulipia huduma ya juu zaidi.
Dkt. Kihamia ameongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa huduma ya mwendokasi inakuwa ya kisasa, yenye uhakika na ya haraka zaidi kwa wakazi wa Dar es Salaam, hasa katika kipindi hiki ambacho jiji linakua kwa kasi na mahitaji ya usafiri yanaongezeka.
Mpango huu unatarajiwa kusaidia kupunguza adha ya foleni na usumbufu wa usafiri wa kila siku kwa maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam, huku DART ikiahidi kushirikisha sekta binafsi zenye uwezo na nia ya dhati ya kuboresha huduma.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!