

Dar es Salaam 24 Julai 2025: Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu waliojitambulisha kutoka mamlaka ya serikali walilazimika kukimbia eneo la tukio baada ya kuyafunga nyororo malori mawili waliyodai yamepaki eneo lisilo sahihi na kutaka kuwatoza faini madereva wake.

Tukio hilo lililokusanya umati wa watu lilitokea pembezoni mwa barabara ya Nyerere eneo la Kituo cha Mafuta cha Victoria ambapo madereva wa malori hayo wakizungumza na Global Tv walisema walifika eneo hilo kwa ajili ya kujaza mafuta kwenye kituo hicho.

Mmoja wa madereva hao alisema wakiwa wanasubiria foleni zao za kujaza mafuta ndipo walipotokea watu hao waliojitambulisha kama maofisa wa serikali wanaohusika na kukamata magari yaliyopaki vibaya.
Hali hiyo ilizua mtafaruku mkubwa kati ya maofisa hao na madereva wa malori hayo jambo lililosababisha Mwenyekiti wa Wamiliki Wadogo na Kati wa Malori Nchini (TAMSTOA), Chuki Shabani kufika eneo hilo na kujaribu kutatua mzozo huo.

Chuki baada ya kufika eneo hilo aliwauliza maofisa hao sababu ya kuyafunga nyororo kwenye matairi malori hayo majibu waliyompa hayakuonekana kumridhisha na kuwataka wamuite bosi wao ili waangalie kwa pamoja kama kuna kosa la msingi la kuyafunga malori hayo.

Mmoja wa maofisa hao alianza kuzungumza na simu na mtu aliyesema ni bosi wake huku akiita “Mkuu… Mkuu…Mkuu… na ghafla afisa huyo na wenzake watatu waliokuwa kwenye Bajaj walionekana kugeuza usafiri wao huo wakitaka kuondoka na kuacha malori hayo yakiwa yamefungwa nyororo.
Kabla ya kuondoka wanahabari wetu waliwauliza sababu ya kuyafunga malori hayo ambapo mmoja wao alisema wao si wasemaji wa tukio hilo na kumtaka mwanahabari wetu kumtafuta Mkurugenzi wao ingawa hakutaka kumtaja jina wala kutoa namba yake.
Baada ya kugoma kuongea afisa huyo na kuona wanahabari na wananchi walichomoka eneo hilo na chombo chao huku wakisema wanakwenda kukamata gari nyingine.
Mpaka wanahabari wetu wanaondoka eneo la tukio hilo maofisa hao walikuwa hawajarudi eneo hilo na wenye malori hayo waliamua kuikata minyororo hiyo na kuendelea na safari zao.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!