Search
Sign In
2Your Cart
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

HUYU HAPA KOCHA MPYA YANGA….JAMAA ALIKUWA ‘AKILI KUBWA’ PALE MAMELOD SUNDOWN…

  • 37
Scroll Down To Discover

YANGA imebakiza hatua ya kumtambulisha tu kocha wake mpya atakayekuja kubeba safari ya kusaka mafanikio zaidi ya mabingwa hao wa soka nchini.

Licha ya kwamba uongozi wa klabu hiyo haujatangaza, lakini taarifa za uhakika nazo ni kwamba kocha anayekuja ni Mfaransa Romain Folz ambaye hana wasifu mzito sana mpaka anatua Yanga.

Wasifu Mkubwa pekee alionao Kocha Folz ni kuwa sehemu ya benchi la ufundi kama kocha msaidizi kwenye kikosi cha Mamelod Sundowns ya Afrika kusini.

Ujio wa kocha kijana Folz mwenye umri wa miaka 35 ndani ya Yanga, utakuwa na presha mbalimbali kupitia rekodi ya klabu hiyo kubwa nchini na yafuatayo yanamsubiri kuthibitisha ubora wake na kama atayafanikisha yatambeba.

Kulinda mataji

Ukianzia kwa kocha Nasreddine Nabi aliondoka akiacha mataji sita, akafuata Miguel Gamondi naye akaacha mataji matatu, Sead Ramovic hakufanikiwa ndani ya muda mfupi lakini Hamdi Miloud naye akaongeza mataji matatu.

Folz ana deni la kwanza hapa kuendeleza ushindi wa mataji, hatua ambayo itaanzia kwa kuyatetea haya yaliyopo. Presha ya wasiwasi inaweza kuanza kumkabili kadri atakavyoshindwa kudumisha ushindi.

Kivuli cha Nabi, Gamondi

Kule Afrika Kusini wamekuwa wakiona Folz hakustahili kupewa kazi ya kuifundisha klabu kubwa kama Yanga, wameshambulia sana lakini Mfaransa huyo anaweza kuwashangaza endapo tu atafanya makubwa kwa kufanya mambo makubwa akiwa Jangwani.

Yanga watampokea kwa shangwe, lakini watakuwa na kiu ya kuona analeta nini cha kuvutia kwani wakati wa Nabi aliunda jeshi la mafanikio, Gamondi akaifanya timu hiyo kupiga mpira mwingi na dozi kubwa za mabao, akafuata Hamdi ambaye naye ndani ya nusu msimu tu akaondoka bila kupoteza mechi hata moja. Kwa msingi huu, kitu kinachosubiriwa ni kuona Folz atafanya nini kuwafikia au kuwazidi watangulizi wake.

Yanga CAF

Hapa ndani ya nchi Yanga imekuwa haizuiliki. Changamoto ambayo mabosi wa Yanga na hata mashabiki wao wanaisubiri kuona inapata tiba ni anga za kimataifa ambako mabingwa hao watarejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025-26 baada kuishia hatua ya makundi msimu uliopita.

Msimu uliopita Yanga ilidai kwamba malengo yake yalikuwa ni kufika hatua ya makundi, lakini ukiangalia uhalisia ni kwamba ilidhamiria kucheza nusu fainali baada ya msimu uliotangulia kufika robo-fainali na kutolewa kiutata na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikionekana ‘kunyimwa’ bao la Stephane Aziz Ki ambalo lingetosha kuwapeleka nusu fainali.

Msimu ujao uongozi umetaka tu kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa ukijipunguzia presha, lakini Folz atapimwa wapi atafika kwenye mashindano haya.

Vita ya Simba, Azam

Msimu uliopita Yanga ilichukua ubingwa kupitia mchezo wa mwisho wa ligi ilipoichapa Simba 2-0 ambayo iliwapa presha kubwa kwenye msimu uliokuwa mgumu.

Kumbuka Yanga iliifunga Simba msimu huo kwenye mechi zote mbili lakini ikapoteza mechi ya kwanza dhidi ya Azam, wakati mabingwa wakiwa chini ya Gamondi kisha wakalipa kisasi dhidi ya wanalambalamba kwa ushindi wakiwa chini ya Miloud.

Msimu ujao, Simba ambayo inajiuliza kwa kugeuzwa kibonde wa Yanga itapambana kurudisha heshima yake mbele ya watani wao hao, lakini Azam nayo itakayokuwa chini ya kocha Florent Ibenge itakuwa na hesabu zake. Hizi ni klabu mbili ambazo bila ya shaka zitakuwa ni mtihani mkubwa kwa Folz katika safari yake kusaka mafanikio.

Mabadiliko ya kikosi

Wakati Yanga ikiwa chini ya Miloud kuna wakati kama mashabiki na viongozi walikuwa hawaelewi mabadiliko makubwa ya kikosi chao, kabla ya hapo kuna ile ‘Gusa Achia, Twende Kwao’ iliyoletwa na Ramovic.

Folz anayehusudu kutumia mfumo wa 4-3-3, staili ya ‘direct football’ na kiu ya kufunga mabao mengi, hata wapinzani watasubiri kuona falsafa zake zinakuja na mabadiliko yapi yatakayoibeba timu hiyo kwenye zama zake ndani ya klabu hiyo yenye presha kubwa ya matokeo.

Kupitia dirisha hili la uhamisho, kuna majina makubwa yanatarajiwa kuondoka katika kikosi miongoni mwao akitajwa, kiungo mhimili wa timu Khalid Aucho, kiungo Aziz Ki (ambaye ameshajiunga na Wydad Casablanca), Kennedy Musonda na wengineo, huku Clement Mzize aliwaniwa na klabu kadhaa. Hii inaweza kuwa mtihani wa kwanza kwa Folz ambaye timu yake imeshasaini wachezaji kadhaa kama Celestin Ecua na Moussa Conte, kujaribu kuwaingiza katika mfumo wa kikosi hicho cha timu ya wananchi.

Hatma ya hayo yote yatakuwa kwenye mikono ya Folz kuanzia pale atakapoanza kazi, akiyafanikisha yatambeba na kuimbwa jina lake, lakini akishindwa presha itakuwa kwake kwani mashabiki wa timu hiyo hawajui kuficha kile wasichokikubali.

The post HUYU HAPA KOCHA MPYA YANGA….JAMAA ALIKUWA ‘AKILI KUBWA’ PALE MAMELOD SUNDOWN… appeared first on Soka La Bongo.



Prev Post PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO JULAI 21, 2025
Next Post BAADA YA KUMALIZANA NA BALLA CONTE….MASHINE HIZI ZA KAZI KUFUATIA YANGA….
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook