

Benki ya CRDB imetangazwa kuwa Benki Bora Tanzania, Benki Bora kwa Masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), na Benki Bora kwa Biashara Ndogo na za Kati (SME) na jarida la kifedha la kimataifa la Euromoney, wakati wa hafla ya kutuza washindi wa Tuzo za Ubora za Euromoney iliyofanyika jijini London Julai 17 2025.
Tuzo hizo zilipokelewa kwa niaba ya Benki na Bi. Tully Esther Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, katika hafla iliyohudhuriwa na zaidi ya wabobezi 500 wa sekta ya benki na fedha kutoka kote duniani. Bi. Mwambapa aliambatana na maafisa waandamizi wa Benki ya CRDB pamoja na wawakilishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Bi. Mwambapa alisema, “Heshima hii ya tuzo nne kutoka Euromoney inadhihirisha dhamira ya msingi ya Benki yetu ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo kwa watu binafsi, wafanyabiashara, na jamii kwa ujumla. Tunapoendelea na kuadhimisha miaka 30 ya Benki ya CRDB, tuzo hizi zinatupa chachu ya kuendelea kusimamia kusudi letu la kuboresha maisha na kuleta mabadiliko chanya ya kudumu katika uendeshaji wetu.”
Tuzo hizi tatu zimekuja miezi miwili tu baada ya Benki ya CRDB kutambuliwa na Euromoney kama Benki Bora kwa huduma za benki zinazofata misingi ya Kiislamu nchini Tanzania kupitia huduma zake za CRDB Al Barakah Banking wakati wa tuzo za Euromoney Islamic Finance zilizofanyika Dubai mnamo tarehe 20 Mei 2025 na kufanya Benki ya CRDB kubeba jumla ya tuzo nne kutoka Euromoney tuzo zenye heshima kubwa zaidi katika sekta ya fedha ulimwenguni.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!