
Serikali imeitaka sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa mpango mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na mpango mkakati huo kutajwa kuwa mkombozi wa misitu na mazingira.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira na Nishati Safi ya Kupikia katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema kuathiriwa kwa mazingira kunatokana na ukataji wa mkaa na kuni hivyo ni muhimu mpango mkakati huo kutekelezwa.
Alisema kasi ya uharibifu wa mazingira inatishia baadhi ya mikoa kukosa uwezo wa kuzalisha chakula kufuatia kukosa mvua na maji ukiwemo Mkoa wa Morogoro.
Mhandisi Luhemeja alisema utekelezaji wa mkakati huo unahitaji mshikamano na uhitaji wa pande zote,Sekta Binafsi,Asasi za kiraia na Viongozi wa Jamii na washirika wa maendeleo kwani vita hii ni watu wote.
”Kama mnakumbuka miaka mitatu iliyopita Dar es Salaam ilikubwa na Changamoto ya maji,mto ulikauka na sababu ya mto kwasababu mvua haikunyesha na maji kupotea mjini,watu walilazimika kununua maji dumu moja mpaka sh.5000 ambapo napo yalikuwa hayapatikani.
”Zote hizi ni changamoto ambazo ni lazima tuzione na ni lazima tuzisimamie,kwani hii dunia hatuirithi kutoka kwa babu zetu bali tunaazima kwaajili ya watoto na wajukuu wetu,”alisema.
Alisema suala la nishati safi ya kupikia wizara ya tumeichukua na kuisapoti sana hivyo aliwataka wadau wa mazingira kuwa mabalozi wa mazingira na kuitangaza mazingira.
Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tantrade, Lulu Mkudde alisema ni muhimu kutunza mazingira.
“Tunatambua jitihada zinazofanywa na serikali katika kutunza mazingira ndiyo maana Tantrade tumeamua kuwa na siku hii kwa sababu mazingira ni kama injini ya maendeleo ya sasa na baadaye kwani inatoa fursa mbalimbali kwa wadau wa biashara,” alisema.
Haya hivyo alisema mabadiliko ya tabianchi yayaoendelea kushuhudiwa duniani yameibua hali ya tahadhari duniani kote na kufungua milango ya ubunifu teknolojia kwa wale wanaotaka kubadili changamoto kuwa fursa.
Baadhi ya fursa zilizopo katoka sekta hii ni kilimo hai na kaboni, utalii wa mazingira uzalishsji na uuzaji wa bidhaa mbadala ikiwemo viroba vya karatasi, teknolojia ya usafi wa mazingira , mafunzo na ushauri wa kimazingira.
Mwakilishi wa Puma Energy, Benidict Ndunguru amesema wamekuwa wakihakikisha wanapunguza matumizi ya kuni katika kupikia ili kupunguza madhara ya moshi kwa kina mama na familia kwa ujumla
“Tuko tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbakimbali ili kufikia lengo la matumizi ya nishati safi Tanzania,” amesema Ndunguru.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!