
Dar es Salaam, Julai 3, 2025 – Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, ametangaza kuwa jumla ya wanachama 5,475 wamechukua fomu kuwania nafasi za Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025.
Akizungumza leo katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Makalla amesema kuwa zoezi hilo la kuchukua na kurejesha fomu lilihitimishwa rasmi hapo jana, Julai 2, 2025.
Kwa mujibu wa Makalla, kwa nafasi ya ubunge katika majimbo yote 272 ya uchaguzi nchini:
Watia nia kutoka Tanzania Bara ni 3,585
Watia nia kutoka Zanzibar ni 524
Wanawake waliojitokeza kugombea ni 263
Aidha, kwa upande wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, jumla ya wagombea 503 walichukua fomu.
Makalla ameeleza kuwa idadi hiyo inaonesha mwitikio mkubwa wa wanachama wa CCM katika kushiriki kuwania nafasi za uongozi ndani ya mfumo wa kidemokrasia wa chama, na kwamba hatua inayofuata ni mchakato wa uchujaji utakaoanza rasmi kesho.
“Tunajivunia kuona wanachama wetu wengi wamejitokeza. Huu ni ushahidi wa imani kubwa waliyonayo kwa chama na mfumo wake wa kiuongozi,” amesema Makalla.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!