
Kampuni ya Airtel Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kupitia mradi wake wa kijamii wa Airtel SmartWASOMI, imekabidhi na kufunga vifaa vya intaneti ya kasi kwa shule 30 za sekondari mkoani Dodoma. Vifaa hivi vitawawezesha walimu na wanafunzi kupata huduma ya intaneti bure, ili kujisomea bure kupitia maktaba mtandaoni ya Taasisi ya Elimu Tanzania na majukwaa ya elimu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mtemi Mazengo, Mkoani Dodoma mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kanda ya Airtel Tanzania Dodoma, Bw. Salum Ngururu alisema, SmartWASOMI siyo tu mtandao, bali ni mfumo wa kidijitali unaoleta vifaa, maudhui ya kielimu yanayolingana na mtaala, na jukwaa la usomaji na ufundishaji wa kisasa
“Mpango huu unaunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano katika kutumia teknolojia ya mawasiliano (TEHAMA) kwenye sekta ya elimu, alisema meneja huyo.
Naye Bi. Grace Samwel akizungumza wa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma,aliishukuru Airtel na kusema, Shule zetu sasa zinaweza kusoma kidijitali kwenye maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu (TET) au kupata maudhui kutoka maktaba mtandao ya Shule Direct bila bila gharama ya bando, tunawashukuru Airtel kwa kuwezesha elimu ya kidijitali kufika hadi kwa wanafunzi wetu bila gharama yoyote.
Pia Airtel imeeleza kuwa mradi wa Airtel SmartWASOMI tayari umeshatekelezwa katika mikoa ya Zanzibar, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mbeya na sasa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuunganisha shule 3,000 nchini kwa kushirikiana na Serikali na UNICEF.
Kwa upande wake, Mwalimu Florian Kashasila alisema; Vifaa vya intaneti ya kasi ya Airtel tulivyopatiwa leo vitasaidia sana walimu na wanafunzi kupata nyenzo za kufundishia na kujifunzia, ambazo awali hazikupatikana kirahisi shuleni.
Airtel Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa sehemu ya mabadiliko ya elimu nchini kwa kuhakikisha shule haziachwi nyuma katika safari ya ujumuishaji wa kidijitali.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!