Search
Sign In
2 Register
Your Cart 2 items
Subtotal : $1559

VYA AZIZI KI VYAPATA MRITHI YANGA….MAYELE ATAJWA UPYAAAA….

  • 9
Scroll Down To Discover

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga Pacome Zouzoua pamoja na straika mpya, Andy Boyeli wameachiwa msala katika kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026.

Pacome anayeitumikia Yanga kwa msimu wa tatu ameachiwa msala wa Stephane Aziz KI aliyetimkia Wydad Casablanca ya Morocco akiwa ameitumia pia kwa misimu mitatu akiifungia jumla ya mabao 39 katika Ligi Kuu.

Aziz alifunga mabao tisa katika msimu wa kwanza wa ligi, kisha akafunga tena 21 akiwa mfungaji bora wa msimu na alipoondoka katikati ya msimu uliopita alikuwa na mabao tisa pia, huku akiwa anaotumia jezi namba 10.

Kwa sasa jezi hiyo amepewa Pacome ambaye misimu miwili iliyopita alifunga jumla ya mabao 19 katika ligi, hali inayomfanya awe na kibarua cha kuibeba Yanga kama ilivyokuwa kwa Aziz Ki.

Pacome alijiunga na Yanga msimu wa 2023-2024 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast alikokuwa mchezaji bora wa msimu (MVP).

Katika msimu wa kwanza, Pacome alipachika mabao saba na asisti tatu akicheza mechi 23 akitumika kwa dakika 1520. Jumla alihusika katika mabao 10 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 80 katika mechi 30.

Msimu uliopita 2024-2025, Pacome alifunga mabao 12 na kutoa asisti tisa na kumfanya kuhusika na mabao 21 kati ya 83 yaliyofungwa na timu hiyo iliyotwaa tena ubingwa wa ligi ikiwa ni mara nne mfululizo.

Hadi anaondoka Yanga, Aziz KI amejipambanua ni mchezaji wa aina gani kutokana na kuwa kinara kwa wachezaji waliofunga hat trick nyingi katika muda mfupi Ligi Kuu Bara akiwa nazo nne na moja Kombe la FA ikifanya jumla kufikisha tano ndani ya misimu mitatu.

Kipindi wakicheza pamoja Aziz Ki na Pacome walikuwa wakitengeneza kombinesheni tishio eneo la ushambuliaji la Yanga, licha ya wote kucheza vyema kama mshambuliaji wa pili nyuma ya straika.

Lakini kuondoka kwa Aziz KI kumempa nafasi Pacome sasa kutawala eneo hilo na katika kunakikisha amerithi kila kitu kwa sasa hata jezi namba 10 aliyokuwa akivaa nyota mwenzake huyo ameachiwa yeye.

Hivyo, kwa sasa Pacome atakuwa na kazi kubwa ya kuiendesha timu na kulisha washambuliaji wenzake na kufunga kama alivyokuwa akifanya Aziz KI ambaye licha ya kufunga mabao 39 ya Ligi Kuu pia aliasisti mara 20 na kumfanya kwa misimu mitatu Jangwani ahusike na mabao 59.

Rekodi zinaonyesha kwa misimu miwili ya kuwa Yanga, Pacome licha ya kufunga mabao 19 ya ligi, lakini ameasisti pia 12, ikiwa na maana amehusika na mabao 31.

KWA BOYELI SASA

Andy Boyeli ametua Yanga dirisha la usajili linalotarajiwa kufungwa mwezi ujao, ana kibarua kizito kutokana na kuichagua jezi namba 9 ambayo ilivaliwa mara ya mwisho na Fiston Mayele aliyeitumikia timu hiyo kwa misimu miwili na kuibeba timu hiyo mabegani mwake.

Mayele ambaye kwa sasa anakipiga Pyramids ya Misri, ndiye aliyekuwa mshambuliaji wa mwisho wa Yanga aliyefunga mabao mengi katika misimu miwili aliyoitumikia.

Katika msimu wa kwanza akivaa uzi wa rangi ya kijani na njano, Mayele alifunga mabao 16 akimaliza kama kinara wa klabu na wa pili katika Ligi Kuu nyuma ya George Mpole aliyekuwa Mfungaji Bora msimu wa 2021-2022 akiitumikia Geita Gold iliyopo Ligi ya Championship kwa sasa baada ya kushuka daraja 2023-2024.

Kwa msimu wa pili wa akiwa Yanga, Mayele alimaliza kama Mfungaji Bora wa klabu na Ligi Kuu kwa jumla akikwamisha wavuni mabao 17 kabla ya Wamisri kumnunua mwishoni mwa msimu, akiweka heshima ya kuifungia jumla ya mabao 33 katika Ligi Kuu.

Pia mabao 14 aliyofunga katika Kombe la Shirikisho Afrika, yakiwamo saba yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano hiyo 2022-2023 iliifanya Yanga kuandika rekodi ya kucheza fainali ya kwanza ya CAF.

Mayele alifanya mambo makubwa akiwa na jezi hiyo namba 9 ambayo ilishindwa kupata wa kuitumikia licha ya kuletwa kwa washambuliaji wengine wa kigeni akiwamo Hafiz Konkoun, Joseph Guede na Prince Dube mbali na Kennedy Musonda aliyecheza kikosi kimoja na kumuacha Jangwani.

Lakini msimu huu, Yanga imemshusha Boyeli kwa mkopo kutoka Sekhukhune United ya Afrika Kusini na straika huyo kuchagua jezi namba 9 akibeba matumaini makubwa ya timu hiyo.

Tayari straika huyo aliyefunga mabao sita msimu uliopita ameanza kuonyesha makeke katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Rwanda dhidi ya Rayon Sport alifunga bao moja na kuasisti jingine wakati Yanga ikishinda 3-1.

Rekodi zinaonyesha straika huyo akiwa na Power Dynamos ya Zambia msimu wa 2022-2023 alitwaa kiatu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zambia baada ya kufunga mabao 18. utokana na mafanikio hayo mwishoni mwa msimu, nyota huyo alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu (MVP).

Msimu wa 2023/24 alifunga mabao manane akicheza mechi 22 za Ligi, huku msimu uliopita raia huyo wa DR Congo akiwa Sekhukhune United ya Afrika Kusini katika mechi 25 alizocheza amefunga mabao sita.

Uamuzi wake wa kuchagua jezi hiyo, ina maana Boyeli ana kibarua cha kuitendea haki namba hiyo na kuachiwa msala wa kazi kubwa iliyofanywa na Mayele wakati akiitumikia timu hiyo iliyotwaa mataji matano kwa mpigo msimu uliopita ikiwamo kutetea la Ligi na Kombe la FA mara nne mfululizo.

Boyeli ametua Yanga akiikuta timu hiyo ina washambuliaji wawili waliofunga jumla ya mabao 27 msimu uliopita, yaani Prince Dube na Clement Mzize aliyeibuka kinara wa mabao wa klabu hiyo akifunga 14. Dube alifunga 13, lakini pia kuna Celestin Ecua aliyetua naye hivi karibuni.

Katika Ligi Kuu ya Ivory Coast akiwa na Zoman aliyoitumikia kwa mkopo kutoka ASEC Mimosas, Ecua alifunga mabao 15 na asisti 12, kitu kinachomfanya Boyeli kuwa na kibarua kizito na kuibeba Yanga katika michuano itakayoshiriki ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la FA, Kombe la Muungano na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo ikipangwa kuanza raundi ya kwanza na Wiliete Banguela ya Angola.

KAMWE ATIA NENO

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ameliambia Mwanaspoti, Zouzoua ni usajili mpya wa jezi namba 10 msimu ujao na ataivaa hadi hapo atakapoamua kutimka ndani ya kikosi hicho, huku akikiri wanaamini atafanya mambo makubwa zaidi ya walivyomzoea.

“Ni kweli (Pacome) kabadilisha namba aliyokuwa anavaa msimu uliopita, sasa atavaa jezi namba 10, hii ni baada ya kuiomba na kimsingi na kibiashara huwezi kuwa na msimu mzima bila kuwa na jezi namba 10 mgongoni,” alisema Kamwe na kuongeza;

“Kila mchezaji tuliyemsajili hakuna hata mmoja aliyekubali, wote wameikataa kwa sababu kuna daraja kubwa la ubora limeachwa na Aziz Ki, hivyo jezi hiyo tuna imani kubwa na Pacome. Hakuna klabu isiyokuwa na jezi namba 10, ina rekodi kubwa na imevaliwa na wachezaji wengi wakubwa akiwemo marehemu Diego Maradona, Lionel Messi, hivyo ni jezi yenye rekodi. Pacome ameiomba na kapewa, hivyo ataanzia alipoishia,” alisema Kamwe.

The post VYA AZIZI KI VYAPATA MRITHI YANGA….MAYELE ATAJWA UPYAAAA…. appeared first on Soka La Bongo.



Prev Post HUKO SIMBA VYUMA BADOOH…..MASHINE MPYA HII HAPA…IMECHEZA KOMBE LA DUNIA LA KLABU…
Next Post NAFASI Za Kazi Kinglion Investment Ltd
Related Posts
Comments 0

    Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!

Leave A Comment
or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook