
Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb, ametembelea mradi maalum wa kuwawezesha wanawake wafanyabiashara wadogo unaofadhili na nchi hiyo kupitia shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women) katika jengo la Machinga Complex, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo Rais Stubb alipata fursa kujionea shughuli mbalimbali za biashara na uzalishaji zinazofanywa na Wanawake wanao nufaika na mradi huo, na kufanyanao mazungumzo. Mradi huo ulioanzwa kutekelezwa mwaka 2022 unawanufaisha zaidi ya wanawake 600 huku ukigahrimu kiasi cha Euro milioni 2 kila mwaka.
Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano na Manispaa ya Ilala vilevile unalenga kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuwajengea uwezo wanawake hao katika njanya mbalimbali kupitia mafunzo ikiwemo usimamazi wa fedha, uongozi, huduma kwa wateja, ujasiriamali mbinu za kisasa za utafutaji masoko, kuboresha bidhaa na usawa wa kijinsia.
Rais Stubb ameleeza kuridhishwa kwake na matokeo ya utelezaji wa mradi huo, kwa unavyowawezesha wanawake kutumia ujasiriamali kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi na kusisitiza kuwa Serikali ya Finland itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Tanzania katika kuwawezesha wanawake kunufaika na fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima, ambaye alimpokea Rais Stubb na ujumbe wake, alimshukuru Rais huyo kwa ufadhili wake katika kuboresha maisha ya wanawake kupitia mikopo midogo, mafunzo ya ujasiriamali na kuboresha miundombinu ya biashara.
“Mradi huu umeleta mageuzi makubwa kwa wanawake wanaofanya biashara hapa Machinga Complex. Leo hii wengi wao wanauwezo wa kusomesha watoto, kupata huduma za afya, na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa familia na taifa,” alisema Mhe. Gwajima.
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Finland nchini Tanzania Mheshimiwa Alexander Stubb inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, huku kipaumbele kikiwa katika biashara na uwekezaji ,maendeleo ya kijamii, na mazingira.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!