

Dar es Salaam, Mei 13, 2025 — Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimepokea taarifa za kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Amani Golugwa, usiku wa kuamkia leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CHADEMA, Golugwa alikuwa anatarajiwa kusafiri leo kuelekea nchini Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (International Democracy Union – IDU) unaoanza kesho.
CHADEMA imeeleza kuwa baada ya kuwasiliana na Shirika la Ndege ambalo Golugwa alitarajiwa kusafiri nalo, walifahamishwa kuwa hakuweza kusafiri.
“Tumejulishwa na mmoja wa watu waliokuwepo eneo la tukio kwamba Mhe. Amani Golugwa alipigwa na polisi na hadi sasa simu zake zote hazipatikani,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chama hicho kimefahamishwa kuwa Golugwa yupo Kituo cha Polisi Kati jijini Dar es Salaam. Mawakili wa CHADEMA wameelekea kituoni hapo kufuatilia sakata hilo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!