MAGAZETI ya Leo Jumapili 04 May 2025
Wakili Peter Kibatala amesema Kuwa kutokana na anayopitia mteja wao gerezani ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amewaambia kuwa kuanzia Jumatatu amekusudia kususia kula chakula kushinikiza haki kutendeka.
Wakili Kibatala ametoa kauli hiyo Jumamosi Mei 3, 2025 akizunguma wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam.
“Natoa taarifa rasmi kwa umma mteja wetu Lissu ataanza kususia kula chakula, siyo kwa sababu nyingine, anataka haki itendeke. Pengine kuanzia siku ya Jumatatu tutatoa taarifa, lakini kwa sasa mjue atasusa kula chakula. Kitakachomtokea wala hatajali,” amesema na kuongeza:
“Lissu ni kiongozi na ni jabali kwenye suala la sheria. Ametufanya wengi kusomea sheria na ni mtu ambaye haogopi kesi, hata sisi tusingekuwapo angeendesha kesi mwenyewe.
“Kwa hiyo atasusia kula chakula hadi hapo haki itakapotendeka. Haki ipi? Sitaki kufanya kosa alilofanya Mwanasheria wa Serikali, lakini mjue ni haki tunayoidai mahakamani.”
Lissu aliyekamatwa na Jeshi la Polisi Aprili 9, 2025, akiwa wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma na kisha kuhamishiwa Dar es Salaam, anashtakiwa kwa makosa ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Kupitia mawakili wake, Lissu anapinga kesi hizo kusikilizwa kwa njia ya mtandao ambapo Mahakama imepanga Mei 6, 2025, kutoa uamuzi iwapo kesi hiyo itandeshwe kwa njia ya mtandao au mshtakiwa apelekwe mahakamani.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!