

Rais wa Russia Vladimir Putin yuko tayari kushiriki katika juhudi za kuleta amani nchini Ukraine, na mashauriano ya kina yanaendelea kati ya Urusi na Marekani.
Hata hivyo, ikulu ya Russia Kremlin imesema kwamba hali ya mzozo huo ni tata mno kiasi kwamba haiwezekani kupata mafanikio ya haraka kama vile Washington inavyotarajia.
“Rais anaendelelea kufuatia njia za kisiasa na za kidiplomasia katika kutafuta suluhu ya mzozo huu,” alisema msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Peskov amesisitiza kuwa malengo ya kimkakati ya Russia ni lazima yatimizwe, huku akieleza kuwa Moscow inapendelea kuyafikia kwa njia ya amani.
Aliongeza kuwa Rais Putin ameonesha utayari wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na uongozi wa Ukraine, lakini hadi sasa hakuna jibu lolote kutoka Kyiv.
“Tunasikitika, hatujasikia tamko lolote linaloashiria utayari kutoka Kyiv. Hivyo basi, hatuwezi kujua kama wako tayari kwa mazungumzo hayo au la,” Peskov alieleza.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye amekuwa akijitambulisha kama mpatanishi wa amani, mara kwa mara ametamka nia yake ya kukomesha “umwagaji damu” unaoendelea katika vita hivyo vya zaidi ya miaka mitatu ambavyo sasa serikali yake inavitazama kama vita vya kati ya Marekani na Russia.
Stori na Elvan Stambuli, GPL
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!