

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dkt. Damas Ndumbaro, ameeleza kuwa wizara yake inaendelea na uratibu na utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambapo hadi sasa kampeni hiyo imetekelezwa katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, huku Dar es Salaam ikiwa ndiyo mkoa pekee uliosalia.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo, Jumatano, Aprili 30, 2025, bungeni jijini Dodoma, Waziri Ndumbaro amelieleza Bunge kuwa kufikia mwezi Juni mwaka huu, kampeni hiyo itaanza rasmi katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kukamilisha utekelezaji wake katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndumbaro amezungumzia pia utekelezaji wa kampeni hiyo Visiwani Zanzibar, akieleza kuwa tayari imefanyika katika mikoa ya Kaskazini Pemba, Mjini Magharibi na Kaskazini Unguja, na kwa sasa inatekelezwa katika mikoa ya Kusini Pemba na Kusini Unguja, ambapo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!