
KATIKA jitihada madhubuti za kuhamasisha afya ya moyo na kuongeza uelewa kuhusu magoniwa ya moyo na mishipa, Hospitali ya Saifee imeandaa mashindano ya Marathon ya Moyo ya Saifee yanayotarajia kufanyika Septemba 28, mwaka huu Viwanja vya Masaki.
Mkurugenzi wa matibabu wa hospitali hiyo, Dk. Abbasali Essajee alisema Marathon hiyo ya moyo halitakuwa tukio la kawaida tu la mbio, bali ni mwito kwa umma kuchukua kwa uzito afya ya mioyo yao.
“Magonjwa ya moyo na mishipa bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani, na tukio hili linakusudia kuelimisha, kuwawezesha, na kuwahamasisha watu kuishi maisha yenye afya bora kupitia mazoezi ya mwili, uchunguzi wa mara kwa mara, na huduma za kinga,” alisema na kuongeza;
“Kwa miaka mingi, Hospitali ya Saifee imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo, ikitoa huduma za kisasa za moyo na kushiriki katika kampeni za kijamii za afya. Kupitia Kitengo Maalum cha Moyo, kampeni za afya ya jamii, Hospitali ya Saifee imefanya uchunguzi wa afya ya moyo kwa maelfu ya watu, imetoa matibabu kwa bei nafuu kwa makundi yaliyo hatarini, na imeandaa warsha za elimu kwa ushirikiano na taasisi za serikali.”
Mkuu wa Uhusiano wa Serikali na Mahusiano ya Umma wa Hospitali ya Saifee, Christina Sintah Manongi, alisema wanaamini kuwa kinga ni muhimu sawa na tiba, Marathon hiyo ni ishara ya dhamira yao ya kuokoa maisha kwa njia ya uelimishaji na hatua za mapema za kinga .
Marathon ya Moyo itakuwa na makundi mbalimbali ya mbio kwa kila kiwango cha uwezo wa mwili, kuanzia kilomita 5 hadi Km 21, pamoja na mbio kutakuwa na sehemu husika kwaajili ya upimaji bure wa moyo na mabanda ya uelimishaji kuhusu afya ya moyo.
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!