

Joto la uchaguzi wa Spika wa Bunge la 13 likizidi kupanda ndani ya vyama vya siasa, Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi, anatarajiwa kuongoza kikao cha wabunge watakapomchagua Spika mpya wa Bunge la Muungano wa Tanzania, iwapo atakuwepo ukumbini siku ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2023, Kanuni ya 9(5), endapo Lukuvi atakuwepo katika ukumbi wa Bunge wakati wa uchaguzi, hatakuwa na mpinzani wa kukalia kiti hicho cha mwenyekiti wa kikao, kutokana na kuwa ndiye mbunge mwenye sifa zinazohitajika zaidi kwa mujibu wa kanuni hizo.
Kanuni hizo zinaeleza kuwa mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi wa Spika lazima awe mbunge ambaye amehudumu kwa muda mrefu zaidi mfululizo na asiwe mgombea wa nafasi hiyo, ambapo Katibu wa Bunge humwalika rasmi kuendesha uchaguzi huo.
Lukuvi, ambaye alianza kulitumikia Bunge mwaka 1995, ndiye mbunge mkongwe zaidi miongoni mwa wabunge wa sasa wa Bunge la 13. Katika Bunge lililopita pia alikuwa na hadhi hiyo, na amewahi kuongoza chaguzi mbili zilizopita za Spika.
Mara ya kwanza ilikuwa Novemba 10, 2020, wakati marehemu Job Ndugai alipochaguliwa kuwa Spika wa sita wa Bunge la Muungano, na mara ya pili ilikuwa Februari 1, 2022, wakati Dkt. Tulia Ackson alipochaguliwa kushika wadhifa huo.
Kwa sasa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mchuano wa kuwania kiti hicho umebaki kati ya Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, na Mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele.
Vyama vingine vya siasa vinatarajiwa kutangaza majina ya wagombea wao kabla ya uchaguzi rasmi kufanyika.











Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kuandika maoni!